Kamati ya Bunge yaridhishwa na hali ya utoaji huduma Mloganzila

 

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI wamewashauri Watanzania kuitumia Hospitali ya Taifa Muhimbili -Mloganzila kutokana na uwekezaji uliofanywa na Serikali wa vifaa tiba, wataalamu na mashine za uchunguzi zilizopo hospitalini hapa.

Kauli hiyo imetolewa leo na Makamu Mwenyekiti, Dkt. Faustine Ndugulile wakati kamati hiyo ilipofanya ziara ya kukagua namna ubora na namna huduma zinavyotolewa hospitalini hapo.

Dkt. Ndugulile ameongeza kuwa uwekezaji uliofanywa na Serikali katika Hospitali ya Mloganzila umeifanya hospitali hiyo kutokuwa na tofauti na hospitali zingine Duniani, hivyo hakuna sababu kwa Watanzania kuchangamkia fursa ya uwepo wa hospitali hiyo ya kisasa na yenye mandhari ya kuvutia hapa nchini.

“Kwa niaba ya kamati napenda kupongeza Prof. Janabi na timu yako ya menejimenti kwa huduma nzuri mnazotoa usiku na mchana, endeleeni kuchapa kazi ya kuwahudumia Watanzania wenzetu,” amebainisha Dkt. Ndugulile.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel amesema uwekezaji uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita imepunguza gharama za Watanzania kwenda nje ya nchi kutafuta huduma za kibingwa na kuwavuta watu kutoka nje nchi kwa ajili ya kupata huduma.

Dkt. Mollel ameongeza kuwa Serikali imeendelea kuweka msukumo katika ubora wa huduma ambapo kwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma nzuri kwa lugha nzuri na inayokidhi kiu ya matarajio ya wananchi wanaohitaji huduma.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji Prof. Mohamed Janabi amebainisha kuwa hospitali hii imeendelea kujikita katika kuboresha na kuanzisha huduma za ubingwa bobezi ikiwemo kuondoa uvimbe kwenye sakafu ya ubongo kutumia matundu ya pua.

Huduma zingine ni pamoja na kuondoa mawe kwenye figo kwa kutumia mawimbi mtetemo, upandikizaji wa figo kwa kuvuna figo kutoka kwa mchangiaji kwa njia ya matundu madogo, kupunguza uzito kwa kutumia puto maalumu (intragastic ballon), kupandikiza nyonga na magoti bandia, upasuaji kwa kutumia matundu madogo (laparoscopy surgeries) na kupandikiza koo bandia.

Chapisha Maoni

0 Maoni