Ubunifu wa mbinu za kuongeza idadi ya watalii na vyanzo vya
mapato nchini kwa kuanzisha mazao mapya ya utalii ni mojawapo ya mikakati
inayopigiwa chapuo kwa msisitizo mkubwa na Wizara ya Maliasili na Utalii chini
ya Waziri mwenye dhamana ya Maliasili Mhe. Angellah Kairuki (Mb).
Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA kupitia
Hifadhi ya Kijereshi iliyopo wilaya za Busega na Bariadi Mkoani Simiyu imetumia
vyema fursa hiyo kubuni aina mpya ya zao hilo la utalii. Zao hilo jipya linatoa
fursa kwa watalii kula chakula Hifadhini "Bush Meal" huku wakitazama
na kufurahia mazingira tulivu na vivutio mbalimbali vilivyopo ikiwa ni pamoja
na kubarizi katika pepo zivumazo zenye kutoa hewa mwanana, mambo yanayomfanya mgeni afurahie muda wake
alioutumia na fedha aliyoitoa kutalii katika hifadhi husika.
Aina hii ya utalii imeonekana kuwavutia wageni wengi katika
hifadhi hiyo ambapo Februari 12, 2024
Kijereshi ilipokoea watalii kutoka Uingereza kwa ajili ya kufanya aina hiyo ya
utalii ambapo muda wote walionekana kuufurahia ikizingatiwa kuwa Hifadhi ya
Kijereshi inatambulika kama "Kiota
cha Mbuni" (The Nest of Ostrich)
katika ikolojia ya Serengeti Masai Mara kwa kuwa na idadi kubwa ya ndege nyuni
aina ya mbuni wanaoipamba hifadhi hiyo.
TAWA inaendelea kuwaalika watanzania wote kutembelea na Kutalii Katika Hifadhi hiyo na Hifadhi nyingine nyingi zilizo chini ya Mamlaka hiyo kwa ajili ya shughuli za utalii.
Na. Beatus Maganja
0 Maoni