Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Mashaka
Biteko ameeleza kuwa vijiji vyote 108 vya Wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe
vimekwishafikishiwa nishati ya umeme kupitia miradi inayotekelezwa na Wakala wa
Nishati Vijijini (REA).
Aidha, amesema kuwa katika Wilaya hiyo peke yake, Serikali
imetumia shilingi bilioni 9.5 kupeleka umeme.
“Tunapeleka umeme katika vitongoji vyote vilivyobaki, ili
watu wote wapate umeme,” ameongeza Dkt. Biteko wakati akizungumza na wananchi
wa kijiji cha Ikwavila wilayani humo, Februari 21, katika hafla ya kuwasha
umeme katika Shule ya Msingi Ikwavila.
Naye Mbunge wa Wanging’ombe ambaye pia ni Naibu Waziri,
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Festo Dugange,
amekiri na kuipongeza Serikali kupitia Wizara ya Nishati na REA kwa
kuvifikishia umeme vijiji vyote 108 vya Wilaya hiyo.
“Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, kati ya
vitongoji 525 tulivyonavyo, watendaji wako wachapakazi tayari wametuletea umeme
katika vitongoji 295,” amesema.
Akieleza zaidi, Dugange amesema kuwa katika Mwaka huu wa
Fedha, Serikali imeanza utekelezaji wa miradi ya REA katika vitongoji vingine
72 huku vitongoji 158 vilivyobaki vikiwa na wakandarasi ambao wanaendelea na kazi.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya umeme
vijijini, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Godfrey Chibulunje
ameeleza kuwa kwa sasa REA inatekeleza jumla ya miradi mitatu katika maeneo
tofauti ya Wilaya ya Wanging’ombe.
Ameitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na REA Awamu ya Tatu
Mzunguko wa Pili, Mradi wa Ujazilizi Fungu la Pili B pamoja na Mradi wa
kupeleka umeme kwenye Vituo vya Afya na Pampu za Maji.
Kuhusu takwimu za Mkoa wa Njombe, ameeleza kuwa jumla ya
vijiji 361 kati ya 381 vimekwishafikishiwa umeme wa REA, sawa na asilimia
94.75.
Aidha, vitongoji 1,148 kati ya 1,836 sawa na asilimia 62.5
tayari vimefikiwa na umeme kupitia miradi mbalimbali ya REA.
Viongozi wengine walioshiriki katika hafla hiyo ya kuwasha umeme ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka, Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe Claudia Kitta na viongozi wengine wa Vyama vya Siasa na Serikali.
0 Maoni