Aliyepewa msamaha wa Rais mwaka jana afungwa jela miaka 30

 

Mahakama ya wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza, imemhukumu kifungo cha miaka 30 gerezani mkazi wa Kijiji cha Bugolola wilayani humo, John Chibuga (31) baada ya kumtia hatiani kwa kosa la unyang'anyi wa kutumia silaha.

Hukumu hiyo imetolewa 22 Februari 2024 na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya wilaya ya Ukerewe, Lucas Nyahega kupitia ushahidi uliotolewa mahakamani hapo, na kujiridhisha pasipo kutia shaka kwamba mshtakiwa ametenda kosa hilo na hivyo kumuhukumu kifungo cha miaka 30 gerezani.

Awali, akisoma shtaka hilo, Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Aidan Nziku amesema mshtakiwa alitenda kosa hilo tarehe 15.12.2023 muda wa saa nane mchana katika kijiji cha Kakerege wilaya ya Ukerewe kwa kumvamia Mdala Mangu (34) akiwa nyumbani kwake na kumkata na panga sehemu mbalimbali ya mwili wake kisha kuiba simu ya mkononi na kukimbia kitendo ambacho ni kinyume na kifungu namba 287A cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu sura 16 toleo la mwaka 2022.

Hata hivyo, mshitakiwa alipopewa nafasi ya kujitetea ili apunguziwe adhabu kutokana na shtaka linalomkabili, aliomba Mahakama impunguzia adhabu kwa sababu alikuwa hana pesa ya kujikimu baada ya kutoka gerezani ndipo akaamua kwenda kupora.

Aidha, Mwendesha mashtaka aliiambia Mahakama  kuwa mshtakiwa ni mtenda kosa wa mara ya pili na aliachiliwa huru kwa msamaha wa Rais tarehe 09.12.2023 kwa kosa la kuvunja duka usiku na kuiba ambapo alitiwa hatiani na Mahakama ya Mwanzo Nansio  na tarehe 15.12.2023 akarudia kutenda kosa.

Mwendesha Mashtaka ameiomba Mahakama hiyo itoe adhabu kali, ili iwe fundisho kwake na onyo kwa jamii hususani wafungwa wanaoachiwa huru kwa msamaha wa Rais.

Kutokana na mshtakiwa huyo kurudia kutenda kosa Mahakama hiyo ya wilaya ya Ukerewe ikamhukumu kifungo cha miaka 30 jela.

Chapisha Maoni

0 Maoni