Watu ishirini na tano (25) wameafariki dunia huku wengine
ishirini na moja (21) wakijeruhiwa katika ajali iliyotokea maeneo ya Ngaramtoni
kibaoni by Pass ikihusisha Lori na magari mengine madogo matatu Wilaya ya
Arumeru Mkoa wa Arusha.
Akitoa taarifa ya ajali hiyo Kamishna wa Polisi Operesheni
na Mafunzo wa Jeshi la Polisi CP Awadhi Juma Haji alipofika katika hospitali ya
rufaa ya Mkoa wa Arusha Mount Meru amesema ajali hiyo ilitokea Februari 24, 2024
muda wa saa 11:00 jioni katika Barabara ya Arusha Namanga ambapo ilihusisha
lori lenye namba za usajili KAC 943 H aina ya Mack lenye tela namba za usajili
ZF 6778 mali ya kampuni ya KAY Construction ya Nairobi Nchini Kenya.
CP Awadhi ametaja idadi ya waliofariki katika ajali hiyo
kuwa ni wanaume (14) wanawake (10) na mtoto mmoja wa kike ambao jumla yao ni
(25) huku akiitaja idadi ya raia wa kigeni waliofariki kuwa ni saba (07).
Katika ajali hiyo pia CP Awadhi ametaja idadi ya majeruhi
kuwa ni 21 kati yao wanaume ni kumi na nne (14) na wanawake ni saba (07), huku
akitaja magari yaliyopata ajali katika tukio hilo kuwa ni T 623 CQF aina ya
Nissan Caravan, T 879 DBY aina ya Mercedes Benz Saloon na gari namba T 673 DEW
aina ya Toyota coaster mali ya shule ya (New Vision School).
Pia, Kamishna huyo wa opereshini na mafunzo ya Jeshi la
Polisi nchini amekitaja chanzo cha ajali hiyo kuwa kuwa ni kufeli breki ya lori
kitendo kilichopelekea lori hilo kuyagonga magari mengine yalikuwa mbele yake
huku akibainisha kuwa Jeshi hilo linaendelea kumtafuta dereva aliyesababisha
ajali hiyo ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake.
Sambamba na hilo Kamishna wa Operesheni na Mafunzo Jeshi la Polisi CP Awadhi, ametoa pole kwa wananchi wa Mkoa wa Arusha na watanzania kwa ujumla na raia wa kigeni waliopoteza ndugu zao katika ajalii hiyo.
Na. Abel Paul- Jeshi la Polisi
0 Maoni