WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Mapindizi
Zanzibar inayoongozwa na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi imeanza utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa
vyuo vitano vya kisasa vya mafunzo ya Amali kote nchini.
Amesema ujenzi wa vyuo hivyo utakamilisha shabaha ya
Serikali kuwa na Chuo cha Amali kikubwa na cha kisasa katika kila wilaya, huku
lengo likiwa ni kuhakikisha vijana wote wanapata ujuzi na utaalamu
utakaowasaidia kukabiliana na ushindani wa soko la ajira ndani na nje ya nchi
hasa katika fani za Uchumi wa Buluu.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo, Jumatano, Januari 10, baada
ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Skuli ya Muungano iliyopo Wilaya ya
Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar. Skuli hiyo ambayo itakuwa na madarasa
41 itagharimu shilingi bilioni 6.1 mpaka kukamilika kwake. Uwekaji huo wa jiwe
la msingi ni sehemu ya shamrashamra za maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi
Matukufu ya Zanzibar.
Pia, Mheshimiwa Majaliwa amemtaka mkandarasi anayejenga
mradi huo ambao ulianza kujengwa Mei 2023 na unatarajiwa kukamilika Aprili,
2024, ahakikishe unakamilika kwa wakati na kwa ubora na viwango
vilivyokusudiwa. “Mwezi Aprili shule hii iwe imekamilika. Tunapoweka malengo ya
ujenzi na tukakubalina muda basi lazima ujenzi huo ukamilike kwa wakati.”
“Kipekee ninampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali
Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kazi nzuri
anayoifanya katika kuyaendeleza na kutekeleza malengo ya Mapinduzi ya Zanzibar
na Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa vitendo. Rais Mwinyi ni kiongozi mwenye
busara, hekima na mchapakazi mwenye kuwatumikia wananchi wake kwa kuwaletea
maendeleo wanayoyataka kwa kasi kubwa.”
Mheshimiwa Majaliwa amesema kila mwananchi ni shahidi wa
mabadiliko makubwa ya kimaendeleo yaliyofanyika Zanzibar katika kipindi kifupi
kwani mbali na maboresho hayo katika
sekta mbalimbali ikiwemo ya elimu, Mheshimiwa Rais Dkt. Mwinyi ameendeleza
umoja, mshikamano, amani na utulivu Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Waziri Mkuu amesema hali hiyo imekuwa kichocheo katika
kutekeleza shughuli mbalimbali ya kuwaletea wananchi Maendeleo. Mwenyezi Mungu amzidishie afya njema hekima
na busara katika kuwatumikia zaidi wananchi. Haya ndio malengo hasa ya mapinduzi.
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Lela
Muhamed Mussa (Mb.), ametumia fursa hiyo kutaja baadhi ya mafanikio
yaliyopatikana upande wa sekta ya elimu katika kipindi cha miaka 60 ya
Mapinduzi kuwa ni pamoja kuongezeka kwa Bajeti ya sekta ya elimu kutoka
shilingi bilioni 265.5 mwaka 2021/2022 hadi kufikia shilingi bilioni 457.2
katika mwaka 2022/2023 sawa na ongezeko la asilimia 72.2.
Amesema kiwango hiko cha bajeti katika historia ya Zanzibar ni kielelezo cha dhamira ya Serikali katika kuendeleza Sekta ya Elimu, ambapo kwa sasa imejipanga kujenga shule 25 za ghorofa katika maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024; ikiwemo shule hiyo ya ghorofa tatu (G+3) ya Muungano.
0 Maoni