Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Angellah Kairuki (Mb)
amesema Serikali inatarajia kupata mapato yanayokadiriwa kufikia dola za
Kimarekani milioni 314 katika kipindi cha miaka 20 kutokana na uwekezaji mahiri
katika maeneo saba (7) yaliyo chini ya
usimamizi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA
Mhe. Kairuki ameyasema hayo leo Januari 03, 2024 katika
hafla ya utiaji saini mikataba ya uwekezaji mahiri (Special Wildlife Investment Concession Areas
- SWICA) kati ya TAWA na Makampuni manne ya uwekezaji yanayofanya shughuli za
utalii ndani na nje ya nchi iliyofanyika
chuo cha utalii cha Taifa (NCT) Jijini Dar es Salaam.
Waziri Kairuki amesema kupitia uwekezaji huo unaokadiriwa
kuwa na thamani ya TZS bilioni 696 wawekezaji watawajibika kuwekeza kwenye
miundombinu katika maeneo yao ya uwekezaji na kuhakikisha wananchi wanaozunguka
maeneo hayo wananufaika na kuona umuhimu wa aina hiyo ya uwekezaji.
Aidha amempongeza Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa
Jamhuri ya Muungano waTanzania kwa kufanya filamu maarufu ya Tanzania The Royal
Tour ambayo imeleta matokeo makubwa kwa kuleta ongezeko kubwa la watalii nchini
Kwa upande wake Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA Mabula Misungwi
Nyanda amesema baada ya upembuzi yakinifu uliofanywa katika nchi za SADC kuhusu
uwezekano wa modeli hii ya biashara
(SWICA), uzoefu ulionesha kuwa modeli hii inajulikana kwa uwezo wake wa
kuwezesha Mamlaka za eneo
lililohifadhiwa kuzalisha mapato endelevu kwa ajili ya uhifadhi na maendeleo.
Aidha, amesema mapato yanayotarajiwa kuzalishwa kwa mwaka ni
mara tisa (9) ya mapato yaliyokuwa yakipatikana awali kwa shughuli za utalii zilizokuwa zikifanyika maeneo
hayo, hivyo ongezeko hili la mapato
linaashiria kwamba mpango wa biashara wa SWICA ni chaguo zuri la kufikia
matumizi bora na endelevu ya rasilimali ya wanyamapori kwa manufaa ya kiuchumi
Pia, amesisitiza kuwa TAWA imejipanga vyema kuhakikisha
inatekeleza vyema miradi yote ya SWICA katika maeneo husika kwa kushirikiana na
wawekezaji
Maeneo ya kimkakati ya uwekezaji mahiri yanayotajwa
kuwekezwa ni Pori la Akiba Mkungunero (Dodoma), mapori ya akiba Ikorongo na
Grumeti (Mara) pamoja na Pori la Akiba Maswa (Kimali, Mbono na Kaskazini)
Mkoani Simiyu.
Aidha, Makampuni
yaliyowekeza katika maeneo hayo ni Bushman Safari Trackers Ltd (Maswa GR
North), Grumeti Reserves Ltd (Grumeti na Ikorongo GR), Mwiba Holdings Ltd
(Maswa GR Mbona na Maswa GR Kimali) pamoja na Kampuni ya Magellan General
Trading LLC (Mkungunero GR).
Hafla hiyo imehudhuriwa na Naibu Waziri wa Maliasili na
Utalii Mhe. Dunstan Kitandula(Mb), Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii,
Dkt. Hassan Abbasi, Mwenyekiti wa Bodi ya TAWA, Mej. Jen. (Mstaafu) Hamis
Semfuko
Wengine ni Makamishna wa Uhifadhi kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na Mamlaka ya Uhifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA), baadhi ya watendaji na maafisa kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na TAWA pamoja na wadau mbalimbali wa uhifadhi.
Na Beatus Maganja, Dar es Salaam
0 Maoni