Ushirikishwaji vikundi vya kijamii kwenye matengenezo ya
barabara ya Kisangara kwenda Shighatini wilayani Mwanga umemfurahisha Mtendaji
Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mhandisi Victor Seff.
Mhandisi Seff amefanya ziara ya kikazi katika Wilaya hiyo
kukagua mradi wa matengenezo katika barabara hiyo yenye urefu wa Km. 25,
unaofanywa na kikundi maalum cha kijamii kiitwacho Muhako Engineering,
kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga Mkoa wa Kilimanjaro.
Mhandisi Seff amesema amefurahishwa sana na ushirikishwaji
huo wa vikundi vya kijamii katika utekelezaji wa miradi katika matengenezo ya
barabara kwani jamii inayozunguka miradi hiyo inapata ajira na kuweza kuinuka
kiuchumi.
Ametumia ziara hiyo, kutoa wito kwa Halmashauri kuwajengea uwezo
na kuhamasisha vikundi vya kijamii ili viweze kufanya kazi za matengenezo ya
barabara ili kufikia asilimia 30 ya bajeti zinazotengwa kwa ajili ya
kazi hizo kila mwaka ambapo
kunawawezesha kuinuka kiuchumi na kuondokana na umasikini.
Naye Mkurugenzi wa ufundi wa Kikundi cha Muhako Engineering
Bw. Stephen Mkeni alimueleza Mtendaji Mkuu kwamba wananchi katika eneo la mradi
wameshirikishwa vyema kwenye kazi zinazoendelea na hivyo wameweza kupata ajira
na kuwawezesha kujikimu kimaisha pamoja na familia zao.
Wakala ya barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) hushirikisha vikundi maalum katika shughuli mbalimbali za matengenezo ya barabara ili kuwezesha jamii kukuza uchumi wao binafsi pia kuhakikisha wanatunza miundombinu inayozunguka maeneo yao.
0 Maoni