Ujenzi wa barabara ya Lupeta-Wimba -Izumbwe yenye urefu wa
Km.9.5 na ile ya Inyala-Simambwe Km. 16.7 kwa kiwango cha lami imelenga
kuchochea ukuaji wa uchumi kwa wananchi mkoani Mbeya kwa kurahisisha
usafirishaji wa mazao kwa urahisi.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Dennis Londo wakati wa ziara ya kukagua miradi ya elimu na miundombinu ya
Barbara mkoani Mbeya.
Mhe. Lundo alisema kuwa kamati hiyo imeridhishwa na
utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa barabara na madaraja chini ya Wakala ya
Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).
"Kazi kubwa na yenye viwango imefanyika katika elimu na
miundombinu katika Halmashauri hii, Miradi hii miwili ya barabara
tuliyotembelea ni muhimu kwa uchumi wa
Mbeya lakini na Taifa kwa ujumla,” alisema Mhe. Londo.
Kwa upande wa uchumi Mhe. Londo alisema barabara hizo
zitaeda kurahisisha shughuli za kilimo na kupunguza gharama za pembejeo na uzalishaji kwani gharama za usafirishaji zitapungua, hivyo kumuongezea kipato mkulima
mmoja mmoja na kumuondolea umaskini mwananchi.
Naye, Naibu Katibu Mkuu anayesimamia Miundombinu Mhandisi
Rogatus Mativila alisema wamepokea maelekezo yote yaliyotolewa na kamati hiyo
na kuahidi kufanyia kazi mapendekezo yote.
Wakati huo huo, Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa TARURA ambaye
pia ni Mkurugenzi wa Barabara Mhandisi Venant Komba alisema kuwa katika Mkoa wa
Mbeya TARURA inaendelea na utekelezaji wa
miradi mbalimbali ikiwemo miradi ya barabara zinazofadhiliwa na Jumuiya ya
Ulaya chini ya mradi wa Agri Connect.
Mhandisi Komba alisema kuwa kwa barabara ya Lupeta-Wimba ipo katika hatua za
mwisho na itakamilika katikati ya mwezi Februari, mwaka huu.
Agri Connect ni mpango unaotekelezwa na TARURA kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU) na madhumuni ya ujenzi ni kukuza uchumi wa Mkoa pamoja na nchi kwa ujumla, kuchochea maendeleo ya sekta binafsi, kutengeneza ajira kwenye sekta ya kilimo na kuongeza thamani ya mazao ya biashara yaliyopo ndani ya Mkoa.
0 Maoni