Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) leo limekabidhi msaada wa
kiutu kwa waathirika wa mafuriko wilayani Kilosa mkoani Morogoro yaliyotokea
hivi karibuni.
Msaada huo wa vyakula na nguo za watoto na wakubwa
umewasilishwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Jukwaa hilo, Jane Mihanji, kwa
niaba ya Mwenyekiti wake, Deodatus Balile, kwa Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka
Hamdu Shaka.
Akikabidhi msaada huo, Mihanji amesema umetokana na kuguswa
kwao na janga hilo lililoleta athari kubwa kwa wakazi wa Kilosa.
Amesema mbali na wao kufanya kazi ya kuhabarisha, kuelimisha
na kuburudisha jamii, kiubinadamu wameguswa na majanga ya asili yaliyowakuta
Watanzania wenzao, hivyo waliamua kuchangishana na kuwasilisha msaada huo
kunakohusika.
Shaka, akipokea msaada huo, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa
Morogoro, Adam Malima, ameishukuru TEF kwa kujitoa kwao.
Shaka ameomba ushirikiano kati ya TEF na Serikali udumishwe,
huku akiwahakikishia wahariri hao kuwa msaada huo utafika kwa walengwa kama
ilivyokusudiwa.
Shaka amesema jamii wilayani Kilosa inatoa shukrani za dhati
kwa wadau waliowafariji waathirika kwani kutoa ni moyo, si utajiri.
Katika makabidhiano hayo TEF iliwakilishwa na Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu, Anita Mendoza; Mjumbe Kamati ya Utendaji Jane Mihanji na Mjumbe Rashid Mtagaluka.
0 Maoni