TARURA imefanikiwa kurejesha mawasiliano ya miundombinu
katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dar es Salaam na hivyo wananchi kuendelea
na shughuli zao kiuchumi na kijamii.
Hayo yamebainishwa na Meneja wa Mkoa wa Dar es Salaam
Mhandisi Geofrey Mkinga wakati wa ukaguzi wa miundombinu katika Wilaya ya
Kinondoni, Temeke na Ubungo.
Mhandisi Mkinga amesema kwamba TARURA imejipanga kukabiliana
na uharibifu uliojitokeza na kutekeleza agizo la Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan
la kuhakikisha mawasiliano yanarejeshwa
na kwamba hakuna shughuli zitakazokwama na kuongezeka kwa gharama za
usafiri kutokana na kukosekana kwa mawasiliano.
“Sisi kama TARURA toka tarehe 21 Januari,2024 tumefanya kazi
kwa 'speed' usiku na mchana na
tutaendelea kuhakikisha shughuli za kiuchumi na kijamii zinarejea kama awali
kwa wakazi wote wa mkoa huu,” amesema Mhandisi Mkinga.
Amesema mvua nyingi zilizonyesha hivi karibuni zilileta
madhara makubwa kwa sababu ya ardhi kujaa maji na kupelekea barabara nyingi
kuathirikia hususan madaraja.
“Mvua zilizonyesha tarehe 20 na 21 Januari, 2024 zilileta
madhara makubwa ambapo kingo za madaraja ziliathiriwa na maji”.
“Madaraja mengi yamebaki mazima lakini maingilio ya daraja
ambayo sehemu ya tuta lake zimesombwa na maji, udongo ulijaa maji hivyo ilikuwa
rahisi kuondoka kila maji yalipokuwa yamezidi kwenye madaraja yetu mengi,”
amesema Mhandisi Mkinga.
Mhandisi Mkinga alitaja madaraja yaliyoathiriwa ni pamoja na
daraja la Ally Hushumu, Mbopo, Madale, Msumi, Tanganyika, Majengo, Bwege pamoja
na daraja la Msumi (Kivule).
Aliongeza Madaraja yaliyoathirika kabisa na hivyo tunahitaji kuyajenga upya hadi hali ya hewa
itakapotulia ni daraja la Msumi-Kivule (Ilala) ambalo limewekwa kivuko cha
watembea kwa miguu pamoja na daraja la Msumi (Madale - Kinondoni) ambalo
watatengeneza kivuko cha watembea kwa
miguu kwani daraja hilo limeharibika
zaidi na haliwezi kutengenezwa kwa haraka.
Aidha, Mhandisi Mkinga alieleza kuwa tayari ujenzi mpya wa
daraja hilo pamoja na Barabara ya Mbezi Msumi – Madale Km 8.5 utafanyika chini
ya Mradi wa DMDP 2 ambao unatarajia kuanza Mei, 2024.
Kuhusu Daraja la Ally Hushumu amesema maingilio yote
yametengenezwa hivyo linapitika kwa sasa.
"Kama mnavyoona huku kuna wanafunzi zaidi ya 250
wanasoma upande mwingine hiyo ndio njia yao ya kwenda shule na pia kuna
watumiaji wengine katika shughuli zao za kijamii,” amesema.
Barabara ya Madale – Bunju ambayo ilikatika sehemu mbili,
Mabanda ya Kuku Km. 8 kutoka Madale na daraja la Mbopo Km. 2 kutoka Madale na
hivyo wananchi wote ndani ya Km. 6 hawakuwa na njia mbadala ya kutumia na hadi
Ijumaa wamesharejeshewa mawasiliano.
“Daraja la Tanganyika lilipo Salasala – Benako ambalo
maingilio yake yalikuwa yamekatika nalo
tumesharejesha mawasiliano na sasa tunaendelea kujaza tuta ili maji yakija tena
yasilete madhara”.
Hata hivyo amesema wamesharejesha barabara ya Salasala-Benako,Goba-Majengo-Kinzudi na kuimarisha maingilio ya daraja la kwa Bwege na njia za kuingilia barabara hizo zimeshakamilika.
Kwa upande wa Temeke jumla ya barabara 15 zenye urefu wa Km.
15.02 na madaraja mawili ziliathirika kwa kiwango kikubwa na wameweza kurejesha
mawasiliano barabara ya Toangoma-Sokoni.
Kigamboni barabara ya Mivomoni iliathiriwa sana hivyo
wamepanga mawe na sasa inatumika ila
wameshampata mkandarasi ambaye atatengeneza barabara hiyo kwa kunyanyua
tuta na kuweka vizuizi vya kuchepusha maji ili iweze kupitika muda
wote.”Barabara ya Dege-Mbutu nayo inasubiri mvua ikatike ili itengenezwe na
iweze kupitika,” aliongeza.
Pia upande wa Ilala-Ukonga Mhandisi huyo amesema
wameshafanyia tathmini barabara za upande huo na sasa wanajipanga kwenda
kufanyia matengenezo barabara ya Banana – Kitunda – Msongola na Kivule
Hospitalini ambazo zipo kwenye mpango wa kujengwa kwa kiwango cha lami kupitia
(DMDP-2) na tatizo la kukosekana mifereji litaenda kutatuliwa.
Kwa Barabara za Ulongoni – Pepeteka – Mwembesupu –
Mwembekiboko - Bangulo km 2.5, Banana – Kitunda – Kivule – Msongola km 9.28, Kitunda - Magore 2.89Km, Kitunda –
Mwanagati – Kwa Mpalange km 6.5, Mombasa - Kivule km 6.84, Mkolemba – Kivule -
Mzunguuko km 1.93, Kwa Diwani - Bombambili km 6.14, Gongolamboto – KIU –Radar -
Majohe 4.35Km, Nguvu Kazi - Yongwe km 6.0, Pugu – Majohe – Mbondole – Njia Nne km 12.2 .
“Hizi zilizopo Jimbo la Ukonga nazo zimeathirika na mvua, zimekwishafanyiwa
tathimini ya maboresho ya kawaida na tunasubiri mvua ipungue tuweze kuanza kazi
ya kurejesha hali ya awali”.
Hata hivyo amesema kutokana na tathmini ya kuangalia maeneo ya Jiji yaliyoathiriwa na mvua Serikali itakuja na mpango wa kujenga mifereji ya mvua na kuondosha hali ya mafuriko na kuzagaa kwa maji katika makazi ya watu kila mara mvua zinaponyesha kwa hali hiyo tatizo hilo itaenda kuondoka.
0 Maoni