Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini
(TARURA) Mhandisi Victor Seff ameagiza Daraja la Mwananchi lililopo Kata ya
Mahina jijini Mwanza kuanza kukarabatiwa
mara moja kufuatia kuharibiwa na Mvua
zinazoendelea kunyesha jijini hapa.
Mhandisi Seff ameyasema hayo jijini Mwanza alipofanya
ukaguzi wa miundombinu ya barabara iliyoharibiwa na mvua zinazoendelea kunyesha
katika Mkoa wa Mwanza.
“Daraja hili la Mwananchi ni kiungo muhimu kwa wafanya
biashara na wakazi wa jiji la Mwanza katika kutekeleza shughuli zao mbalimbali za
kijamii na kiuchumi , hivyo nakuagiza Meneja uanze ukarabati wa daraja hili
mara moja,” aliagiza Mhandisi Seff.
Wakati huo huo Mhandisi Seff ameelekeza Km. 4.5 za barabara
ya Igongwe-Isanzu-Kabusungu wilaya ya Ilemela ziweke kwenye kipaumbele
cha bajeti kwa ajili ya kujengwa kwa kiwango cha lami.
Barabara hiyo yenye urefu wa Km. 5.8 inayoelekea hospitali
mpya ya Wilaya ya Ilemela ambapo Km. 1.3
zipo kwenye ujenzi wa kiwango cha lami.
“Ujenzi wa barabara hii utawarahisishia wananchi wa Ilemela
kupata huduma za afya kwa wakati na kupunguza madhara na vifo
vilivyokuwa vinatokana na kuchelewa kufika kupata huduma katika vituo
vya afya kutokana na ubovu wa miundombinu ya barabara”.
Akiwa katika Halmashauri ya Sengerama, Mhandisi Seff
alitembelea na kujionea ubovu wa barabara uliotokana na mvua katika barabara ya
Tabaruka-Nyibanga-Kishinda Km.11 na Ibondo-Kasongamile-Chamabado Km. 35 na
kumuelekeza Meneja wa TARURA Mkoa wa Mwanza
Mhandisi Makori Kisare kufanya tathimini
ya uharibifu huo.
“Fanyeni tathimini ya uharibifu wa barabara hizi na muweze
kurudisha mawasiliano kwa kufanya
matengenezo ya maeneo korofi na kujenga Makalavati ili barabara hizi ziweze
kupitika katika misimu yote ya mwaka, ” alisisitiza Mhandisi Seff.
Vile vile, Mtendaji Mkuu huyo amewataka Mameneja wa Mikoa wote wa TARURA nchi nzima kufanya ukaguzi wa madaraja na mifereji kabla ya Majira ya mvua kuanza ili kupunguza au kuondoa kabisa madhara na uharibifu wa miundombinu ya barabara pindi mvua zitakaponyesha.
0 Maoni