BARA 18 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema kuwa “Kila raia anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali nchini na duniani kote ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi, na pia juu ya masuala muhimu kwa jamii”. Hivyo suala la wananchi kupata habari ni muhimu kwani ni chachu ya maendeleo na pia ni takwa la kikatiba.
Ni ukweli usiopingika kuwa huduma bora za mawasiliano ni
muhimu sana kwani ni kichocheo katika kuleta maendeleo ya jamii na nchi nzima
kwa ujumla na umuhimu huo unadhirika kutokana na mchango wake katika nyanja za
kiuchumi, kisiasa, kijamii na pia katika masuala ya ulinzi na usalama.
Vilevile, huduma ya mawasiliano ni chachu ya ukuaji wa sekta
nyingine za kiuchumi kutokana na ukweli kwamba mafanikio katika sekta
mbalimbali huchangiwa kwa kiasi kikubwa na uwepo wa huduma za uhakika za
mawasiliano.
Hatua hiyo inatokana na maboresho makubwa yaliyofanywa na
Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan katika sekta hiyo, akiamini kwamba kupitia mawasiliano taarifa
mbalimbali muhimu za Serikali na sekta binafsi zinawafikia walengwa wote
wakiwemo wananchi kwa wakati na kwa ufanisi na hatimaye kuleta tija
inayokusudiwa.
Januari 6, mwaka huu, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alizindua
studio za Redio Jamii- Ruangwa ambayo itaharakisha maendeleo ya wana Ruangwa.
“Tukio la leo ni hatua muhimu katika kuwapatia wananchi haki yao ya kikatiba ya
kupata habari. Ni matumaini yangu kwamba Wana-Ruangwa pamoja na wananchi wa maeneo
jirani watanufaika na huduma za utangazaji zitakazopatikana kupitia redio hii.”
Mheshimiwa Majaliwa alisema Sekta ya utangazaji ni muhimu
sana katika dunia ya sasa ya kidigitali ambapo upashanaji wa habari umekuwa ni
msingi wa ukuaji wa uchumi na kuwa chachu ya maendeleo ya mtu mmoja mmoja na
Taifa kwa ujumla.
“Huu ndio msukumo wa Serikali yetu katika kuhakikisha uwepo
wa miundombinu bora ya mawasiliano yatakayowezesha jamii yote ya Watanzania
kupata habari muhimu za kijamii, kitaifa na kimataifa ambazo zitawapa maarifa
na utayari wa kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo ya Taifa letu.”
Alisema redio hiyo inakusudiwa kusikika katika maeneo ya
Wilaya ya Ruangwa, kutokana na uwezo wa mitambo masafa yatafika hadi maeneo ya
wilaya za Masasi, Liwale na Kilwa, hivyo kuwawezesha wananchi wengi zaidi
kufikiwa na huduma hiyo muhimu kwani kupitia matangazo ya redio hiyo wataweza
kufahamu mambo yanayoendelea katika sehemu mbalimbali nchini na duniani kwa
ujumla.
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa alisema ilani ya Uchaguzi ya
Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2020/2025; Ibara ya 125 (a) imeielekeza Serikali
kuendelea kutekeleza Sheria ya Huduma za Habari na. 12 ya Mwaka 2016 ili
kuhakikisha kuwa wananchi wanapata taarifa sahihi kwa urahisi zaidi na kwa
wakati.
Chanzo: Ofisi ya
Waziri Mkuu
0 Maoni