Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu
Hassan ameridhia kuanza kwa utekelezaji wa kufikisha mradi wa maji wa ziwa
Victoria katika Halmashauri ya Ushetu.
Waziri wa Maji Mhe Jumaa Aweso ameyasema hayo leo tarehe 9
Januari 2024 wakati akizungumza na wananchi wa Busenda katika kata ya Chona,
wilayani Kahama mkoa wa Shinyanga.
Waziri Aweso amesema kuwa tayari amefanya mawasiliano na
watendaji na tayari tenda ya utekelezaji wa mradi wa maji imeshatangazwa ndani
ya siku 30 mkandarasi atakuwa amepatikana na kazi itaanza.
Pia, Waziri Aweso amezindua mradi wa maji wa maji Busenda
ambao umegharimu kiasi cha Shilingi 344,480,060 ikiwa ni fedha zinazotokana na
mpango wa malipo kwa matokeo (PforR) huku akimpongeza Mhandisi wa RUWASA mkoa
wa Shinyanga kwa kusimamia kwa weledi mradi huo.
Waziri Aweso amesema kuwa ujenzi wa mradi huo ni kutokana na
changamoto ya kukosekana kwa huduma ya maji safi na salama na ya uhakika katika
kijiji cha Busenda.
Mbunge wa Jimbo la Ushetu Mhe Emmanuel Cherehani amemshukuru
Mhe Rais Samia Suluhu Hassan kwani mradi huo utasaidia kumtua ndoo mama
kichwani na kumuongezea muda wa kushiriki katika shughuli mbalimbali za
kiuchumi na kijamii pamoja na kupunguza maambukizi ya magonjwa yanayosababishwa
na matumizi ya maji yasiyo salama.
Wananchi wapatao 3,551 watanufaika na huduma ya majisafi na
salama, Mbunge Cherehani amempongeza Rais Samia kwa kukubali kutoa fedha za
ujenzi wa miradi ya maji katika wilaya ya Kahama.
Mhe Cherehani ameitaja changamoto kubwa katika jimbo hilo
kuwa ni ukosefu wa maji kwani kata 11 kati ya 20 hazijafikiwa na mradi wa maji
hivyo mradi wa maji ya ziwa victoria utakuwa muarobaini wa kadhia hiyo.
Utekelezaji wa mradi wa Maji Busenda umefanywa na wataalamu wa ndani wa RUWASA kwa mfumo wa Force Account ambapo utekelezaji wake ulianza rasmi tarehe 10 Machi 2023 na kukamilika tarehe 5 Septemba 2023.
Na Mathias Canal- Ushetu-Kahama
0 Maoni