Mwanamke apandishwa kizimbani kwa tuhuma za mauaji

 

Mwanamke mmoja anaitwae Pili Selenge (47) mkazi wa Wilaya ya Nyamagana Jijini Mwanza amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Ilemela mkoani hapa na kusomewa shtaka la mauaji.

Mshtakiwa huyo amesomewa shtaka hilo tarehe 9 mwezi huu katika kesi ya jinai namba 640/2024 ambapo anadaiwa kumuua mwanaume mmoja asiyefahamika majina wala miaka yake kitendo ambacho ni kinyume na kifungu namba 196 na 197 ya Sheria ya Kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2022.

Akisoma mashtaka hayo mbele ya Hakimu, Fortunatus Kubaja, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Monica Mweli amesema mshtakiwa alitenda kosa hilo Desemba 20 mwaka 2023 eneo la Nyahonze, wilayani Ilemela mkoani Mwanza.

Baada ya kusomewa shtaka hilo, mshitakiwa hakutakiwa kujibu lolote  kutokana na Mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka kisheria ya kusikiliza kesi hiyo, na shauri hilo limeahirishwa hadi Januari 22, mwaka 2024 huku mshtakiwa akipelekwa rumande katika gereza Kuu la Butimba Jijini Mwanza.

Chapisha Maoni

0 Maoni