Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) inatarajia
kuanza usanifu wa daraja la kudumu la chuma (Mabey Bridge) litakalojengwa ili
kuunganisha vijiji vya Nyali na Nzumbo katika kata ya Ulaya-Mikumi Wilayani
Kilosa.
Hayo yameelezwa na Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Victor
Seff wakati akiongea na wananchi wa kata hiyo kwenye ziara yake ya kikazi ya
kukagua hali ya miundombinu wilayani Kilosa.
“Nitawatuma wataalamu wangu wa TARURA Makao Makuu waje
wafanye usanifu wa ujenzi wa daraja la kudumu la chuma ili kuunganisha vijiji
hivi vya Nyali na Nzumbo,”alisema Mhandisi Seff.
Pamoja na hilo, amemwelekeza Meneja wa TARURA Mkoa wa
Morogoro kuanza mara moja ujenzi wa daraja la watembea kwa miguu (Kiteputepu)
ili wananchi wa vijiji hivyo waendelee kupata huduma mbalimbali za kijamii na
kiuchumi.
Vile vile, Mhandisi Seff ameelekeza kufanyika kwa tathimini
ya uharibifu wa barabara za Mikumi ili ziwekwe kwenye mpango wa dharura wa
kurudisha mawasiliano haraka iwezekanavyo.
Awali, Mbunge wa Jimbo la Mikumi ambaye pia ni Mwenyekiti wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge - TAMISEMI Mhe. Dennis Londo amesema barabara nyingi
za Jimbo la Mikumi zimeharibika vibaya kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha
na kuiomba TARURA kuangalia uwezekano wa kukarabati hasa barabara za
Kivungu-Kilangali Km. 1.5, barabara ya Miyombo-Dodoma Isanga Km. 10 pamoja na
ujenzi wa daraja la kudumu la Nyali-Nzumbo.
Daraja la watembea kwa miguu katika mto Nyali ambalo linaunganisha vijiji vya Nyali na Nzumbo litajengwa kufuatia lile la awali kuvunjika.
0 Maoni