Kamati ya kudumu ya Bunge, Ardhi, Maliasili na Utalii
imeeleza kuridhishwa kwake na utekelezaji wa miradi ya mpango wa Taifa wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano
dhidi ya UVIKO - 19 iliyotekelezwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori
Tanzania (TAWA) ndani ya Pori la Akiba Wami Mbiki Mkoani Pwani.
Akizungumza mara baada ya kutembelea na kukagua miradi hiyo, Mwenyekiti wa Kamati Mhe. Timotheo Mzava amempongeza Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ubunifu wake
wa kutafuta fedha na maelekezo aliyoyatoa juu ya matumizi ya fedha za UVIKO
ambazo zimeleta mapinduzi makubwa katika sekta ya utalii.
"Kwa mazingira na hali tuliyoiona (Pori la Akiba Wami
Mbiki) nadhani tutaungana sote kumpongeza kwa dhati kabisa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mama yetu Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri
anayoifanya kwenye Nchi yetu lakini hasa kwa ubunifu mkubwa alionao wa kutafuta
fedha lakini pia maelekezo aliyoyatoa Juu ya matumizi ya fedha za UVIKO "
Mhe. Timotheo Mzava ameelekeza pia pongezi za Kamati yake
kwa Wizara ya Maliasili na Utalii na TAWA kwa kazi nzuri waliyoifanya katika
kusimamia miradi hiyo ambayo iligharimu zaidi ya TZS bilioni mbili.
Sanjari na pongezi hizo, Kamati hiyo imetoa wito kwa TAWA
kuongeza mikakati ya kibiashara na ya kimasoko ikiwa ni pamoja na kutangaza
hifadhi hiyo ili miundombinu iliyotengenezwa iweze kutumika kama ilivyokusudiwa
na Serikali kupata tija inayotarajiwa
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Malialisi na Utalii Mhe.
Dunstan Kitandula (Mb) amesema Wizara imejipanga kuhakikisha inaongeza jitihada
katika kutangaza hifadhi hiyo ili kuongeza idadi ya wageni ikiwa ni pamoja na
kutafuta wabia wa kushirikiana nao katika kuendesha shughuli za utalii na
uwekezaji
Awali akifafanua hoja zilizoibuliwa na baadhi ya wajumbe wa
Kamati hiyo kuhusu mikakati ya TAWA katika kuchechemua utalii katika hifadhi ya
Wami Mbiki, Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA Mabula Misungwi Nyanda amesema TAWA
imekuja na mpango mahsusi wa kufufua hali ya hifadhi hiyo kwa kumtafuta
mwekezaji ambaye atawekeza kituo cha kuokoa na kulea Wanyamapori wenye mahitaji
maalumu (Wildlife Rescue and Rehabilitation Centre).
Amesema tayari TAWA imekwisha saini mkataba na mwekezaji
huyo ambao unatarajiwa kuleta manufaa makubwa kwa Wanyamapori wenye mahitaji
maalumu kama vile wagonjwa, yatima, walionusurika katika matukio ya ajali na
wanyamapori wanaotelekezwa na wazee wanaohitaji uangalizi maalumu.
Aidha, amesema uwepo wa kituo hicho katika hifadhi ya Wami
Mbiki utakuza utalii wa ndani na wa nje kupitia program mbalimbali
zitakazoendeshwa ikiwemo program ya watalii wa kujitolea, utalii wa matukio
lakini pia mwekezaji ameahidi kuleta wageni kati ya 30 mpaka 50 Kila mwezi
jambo ambalo litachagiza utalii katika hifadhi hiyo.
Miradi iliyotembelewa na kukaguliwa na Kamati ya Bunge, Ardhi, Maliasili na Utalii katika ziara hiyo ni pamoja na barabara yenye urefu wa kilometa 47.2, mabanda ya kulala wageni, lango kuu la kuingilia wageni linalojumuisha maduka ya kuuza bidhaa za utalii (Curio shops), jengo la kupumzikia wageni, jengo la kutoa taarifa kwa wageni (Visitors' Information Center), kituo cha mauzo, vyoo pamoja na nyumba za kuishi Maafisa na Askari watakaokuwa wakihudumia wageni.
Na. Beatus Maganja
0 Maoni