Waziri Silaa asimamisha matumizi ya kituo cha mafuta cha Barrel

 

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa amesimamisha matumizi ya Kituo cha Mafuta cha Barrel Petrol Energy cha Mikocheni, Dar es Salaam na kupiga marufuku ujenzi holela wa vituo vya mafuta nchi nzima vinavyojengwa kwenye makazi ya watu hatua inayohatarisha usalama wa watu na mali zao. 

Waziri Silaa ametoa agizo hilo jana alipoenda kukagua eneo kilipojengwa kituo hicho na aliambatana na Kamati ya ulizi na usalama ya Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

"Kufuatia agizo hili, nawaagiza wakuu wote wa Idara ya Ardhi na Mipango Miji nchi nzima wafanye uhakiki wa vituo vya mafuta kwa maana ya viwanja, mabadiliko ya matumizi ya ardhi, mchakato uliotumika, ukubwa wa viwanja, ukaribu wa kituo kimoja na vituo vingine na ukaribu wa maeneo mengine ya kutolea huduma za jamii, hali ya uendeshaji wa vituo hivyo, taarifa hiyo ifike ofisini Januari 31, 2024," amesema Waziri Silaa. 

Pia, Waziri Silaa amewaagiza wafanyabiashara ya mafuta nchini wafanye uhakiki wa vituo vyao na Mafuta, mchakato wa namna walivyopata ardhi wanayotumia na kuwasilisha taarifa hiyo Ofisini kwake ifikapo Januari 31, 2024. 

Aidha, Waziri Silaa amesema ni vema watumishi wa Ardhi na wafanyabiashara hiyo waheshimu Sheria za nchi kwa vitendo kwa kuwasikiliza watu wasio na sauti ili wapate haki zao katika masuala ya ardhi. 

"Rais Samia Suluhu Hassan ni mtu wa haki, anataka watu wapate haki, ameniteua mimi kusimamia haki, hebu tusimamie Sheria, kwa mdomo tukisema tunamuunga mkono Dkt.Samia Suluhu Hasan, lakini tufanye kwa vitendo kwa kuwasililiza wale 'the voiceless, sisi tumewekwa hapa kuwa voice of the voiceless," amesema Waziri Silaa. 

Naye mkaazi wa eneo hilo la Mikocheni Bw. Stephen Rupia amesema wananchi wa eneo hilo hawakushirikishwa kwenye hatua yoyote ya kubadili matumizi ya kiwanja ambayo ilitakiwa wananchi washirikishwe. 

"Tupo hapa eneo hili lilikuwa na ukuta na miti mbele na lilikuwa eneo la mtu kwa matumizi yake, hatukuona bango la kubadilisha matumizi ya eneo hili kujenga kituo hiki cha mafuta," amesema Bw. Rupia. 

Akizungumza kwa niaba ya mmiliki wa kituo hicho cha Mafuta Mhandisi Stanley Kitundu amesema wameyapokea maelekezo ya Waziri Silaa mwenye dhamana ya ardhi na watayatekeleza na kuongeza kuwa kituo chao kimekamilika kwa asilimia 100 lakini kilikuwa hakijaanza kufanyakazi.

Chapisha Maoni

0 Maoni