WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewasili wilaya ya Hanang
mkoani Manyara na kukutana viongozi wa mkoa huo na wa Serikali na kupokea
taarifa ya hali halisi ya tukio la maafa lililotokea jana na kusababisha vifo
na majeruhi.
Waziri Mkuu alitoa pole kwa viongozi na wananchi wa Hanang
kwenye kikao kilichofanyika leo (Jumatatu, Desemba 4, 2023) kwenye ukumbi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Hanang na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo
Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, vyombo vua ulinzi na usalama na
Watendaji wa taasisi za Serikali.
Waziri Mkuu amesema tukio la jana linafanana na tukio
jingine lililowahi kutokea mwaka 1990 katika eneo la Ndanda ambako mlima
uliporomoka na kusomba nyumba na barabara, hali ambayo ilisababisha vifo na
majeruhi.
Amezishukuru Kamati za Maafa za Wilaya na Mkoa ambazo
zilianza kuchukua hatua za uokoaji tangu jana, lakini pia mawaziri na watendaji
wao ambao walikuja kutoa msaada kwa kuungana na viongozi wa mkoa wa Manyara.
Amesema matibabu yanaendelea kutolewa kwa majeruhi ambapo
timu ya madaktari bingwa kutoka Dodoma, Singida na Arusha imeungana na kuanza
kutoa huduma za upasuaji kwa wagonjwa watatu waliovunjika mifupa.
Amesema majeneza yameagizwa kutoka Babati na Singida ili
ndugu waliotambuliwa waweze kuhifadhiwa kwenye nyumba zao za milele.
Hivi sasa, Waziri Mkuu na baadhi ya mawaziri wamekwenda
kukagua eneo la Mlima Hanang kwa kutumia helikopta. Eneo hilo ndiko maporomoko
ya udongo yalianzia. Baadaye atashiriki kuaga miili ya marehemu na ndipo
taarifa rasmi itatolewa.
0 Maoni