Waziri Mkuu, Mhe. Kassim
Majaliwa akisalimiana na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Itikadi na Uenezi,
Paul Makonda, leo Novemba 02, 2023 ofisini kwa Waziri Mkuu, Bungeni Jijini
Dodoma.
KATIBU wa Halmashauri Kuu ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM), Itikadi na Uenezi Paul Makonda amesema CCM haina
shaka na utendaji kazi wa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwani ni kiongozi
mchapakazi na mtiifu.
“Katika utendaji wa kazi
sisi upande wa Chama tuna matumaini makubwa na uwajibikaji na uaminifu wa
Waziri wetu Mkuu Kassim Majaliwa, tumemuona katika maeneo mengi akisimamia
shughuli mbalimbali za Serikali na nilipotoa agizo la Chama kwa Waziri Mkuu
nilitaka agizo hilo lifike kwa mtu anayeweza kuleta matokeo chanya kwa Chama.”
Katibu huyo wa Itikadi na
Uenezi amesema lengo la CCM chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Rais Dkt. Samia
Suluhu Hassan ni kuhakikisha Serikali inatimiza kile ambacho imepewa kukifanya
kwa mujibu wa ilani ya uchaguzi, hivyo wana matumaini makubwa na utendaji kazi
wa Mheshimiwa Majaliwa.
Ameyasema hayo leo
(Alhamisi, Novemba 2, 2023) alipokwenda ofisini kwa Waziri Mkuu Bungeni jijini
Dodoma. Amesema lengo la Chama ni kuhakikisha ndoto ya Mheshimiwa Rais Samia
Suluhu Hassan na kuwatumikia na kuwaletea maendeleo wananchi wote hususani
wanyonge inafikiwa.
Amesema Waziri Mkuu ni
mtendaji mtiifu, mwaminifu na kwamba maelezo yaliyotolewa kwake na CCM kuhusu
kushughulikia migogoro ya ardhi tayari ameyapokea na ameanza kuyatekeleza.
“Nina imani hata miezi sita tuliyompa inawezekana akatumia hata miezi mitatu
tukapata ripoti.”
Kadhalika, Makonda amesema
Chama kimemwagiza Waziri Mkuu kuwachukulia hatua wote ambao wataonekana kukwamisha
utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ndani ya Serikali. “Yeyote ambaye anabainika
kufanya ubadhirifu wa mali za umma na Waziri Mkuu akabaini achukue hatua mara
moja na Chama tumempa baraka zote.”
Kwa upande wake, Waziri Mkuu
amesema Serikali imepokea maelekezo ya Chama na kwamba itaendelea kuyafanyia
kazi na kuhakikisha migogoro ya ardhi katika maeneo mbalimbali nchini
inaendelea kushughulikiwa.
Akizungumzia kuhusu suala la
udhibiti wa fedha za umma, Mheshimiwa Majaliwa amesema serikali itaendelea
kulisimamia jukumu hilo ili fedha zinazotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa
miradi mbalimbali ya maendeleo zitumike ipasavyo na katika viwango vya ubora
vinavyotarajiwa.
0 Maoni