Kutokana na mvua za vuli na masika zinazoendelea hapa nchini,
wito umetolewa kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari za kiafya ikiwemo kudumisha
usafi wa mazingira katika maeneo yao ili kuzuia magonjwa ya mlipuko kama vile
ya kipindupindu na mengineyo.
Wito huo umetolewa Jijini Dodoma na Mkurugenzi Msaidizi
Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma, Wizara ya Afya Dkt. Tumaini Haonga ambapo
amesema mvua zinaponyesha kuna uwezekano wa athari za afya zinazoweza
kujitokeza ikiwemo uharibifu wa miundombinu ya majitaka hali inayoweza
kusababisha kusambaa kwa magonjwa ya mlipuko.
“Kutokana na mvua
zinazoendelea kunyesha, kuna athari za kiafya zinazoweza kujitokeza
ikiwemo uharibifu wa miundombinu ya
majitaka ambayo yanaweza kuchangia au kuibua kusambaa kwa magonjwa ya mlipuko
kama vile ugonjwa wa Kipindupindu lakini kuongezeka kwa magonjwa
yanayosababishwa na minyoo, homa ya matumbo, kwa hiyo nitumie fursa hii kutoa
wito kwa wananchi wenzangu na jamii kwa ujumla
kwa kipindi hiki mvua zinaendelea katika maeneo mbalimbali wazingatie
kanuni za afya kwa kudumisha usafi wa mazingira na kuepusha maji kutuama kwenye
maeneo ya makazi” amesema Dkt. Haonga.
Ikumbukwe kuwa kutokana na utabiri wa hali ya hewa
uliotolewa na Mamlakaya Hali ya Hewa nchini,uwezekano wa kuwepo kwa Mvua juu ya
Wastani uwepo wa El Nino kuanzia sasa
hadi Januari 2024 hasa katika mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga,
Simiyu, Mara, Kigoma, Morogoro, Pwani , Dar es Salaam, Tanga, Arusha, Manyara,
na Kilimanjaro, Wizara ya Afya imekuwa mstari wa mbele kutoa elimu ya afya
ikiwemo wazazi na walezi kuwa makini na
watoto kipindi chote ambacho mvua zitakuwa zinanyesha, watoto kutoruhusiwa
kucheza kwenye mvua au maji na kutocheza kwenye kingo za mito kwani kuna
uwezekano wa kubomoka na kusababisha mtu kuteleza na kusombwa na maji.
Na. Elimu ya Afya kwa Umma
0 Maoni