TAWA kuiingiza mapato makubwa kupitia Makuyuni Wildlife Park

 

Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TAWA Dk. Simon Mduma amesema mpango mkatati wa kibiashara wa kuendeleza shughuli za utalii eneo la Makuyuni Wildlife Park uliondaliwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA unatarajiwa kuiingizia Serikali mapato makubwa ikiwa ni pamoja na kunufaisha jamii zinazozunguka eneo hilo.

Dk. Mduma ameyasema hayo Novemba 26, 2023 wakati wa ziara ya wajumbe wa bodi ya Wakurugenzi ya TAWA katika Hifadhi ya Makuyuni Wildlife Park iliyopo wilaya ya Monduli, Mkoa wa Arusha ikiwa ni mara ya kwanza kwa wajumbe wa bodi hiyo kufanya ziara katika hifadhi tangu ikabidhiwe kwa TAWA Oktoba 03, 2023.

Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi ya TAWA Mej. Jen. (Mstaafu) Hamis Semfuko, Dk. Mduma amesema tangu eneo la Makuyuni Wildlife Park likabadhiwe kwa TAWA, menejimenti ya TAWA imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kuandaa mpango maalumu wa biashara na kuendeleza eneo hilo ili liweze kutumika vizuri kwa biashara ya utalii na mpango huo uliwasilishwa kwenye bodi na bodi ikaridhia utekelezaji wake.

Aidha, amesema pesa kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huo ipo na imekwisha tengwa kilichobaki ni kuanza utekelezaji.

Pia ametoa rai kwa wananchi wanaoishi pembezoni mwa eneo hilo kuongeza ushirikiano kwa TAWA kwa kuwa mradi huo ni wa Taifa na umma kwa ujumla na wao kama wananchi wa eneo husika ni wanufaika wakubwa wa mradi huo.

Kwa upande wake, Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA Mabula Misungwi Nyanda amesisitiza kuwa TAWA itahakikisha inawashirikisha wananchi wote wa Makuyuni katika shughuli zote zitakazofanyika eneo hilo, lakini kwa kuanzia TAWA itaanza zoezi la kuainisha mipaka ili ijulikane kwa wananchi wote

Kamishna Mabula amesema katika eneo hilo kutakuwa na kazi nyingi zitakazofanyika ambazo zitawanufaisha wananchi hasa katika upande wa ajira kama vile ujenzi wa miundombinu ya barabara, malazi ya watalii n.k.

Aidha, amewapongeza wanahabari wote nchini kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kutangaza utalii na shughuli mbalimbali zinazofanywa na TAWA nchini.

Naye Kamanda wa Makuyuni Wildlife Park Andrew Kishe amesema katika kipindi cha mwaka mmoja wa kukabidhiwa kulilinda eneo hilo hali ya usalama wa Wanyamapori imeimarika sana na kupelekea ongezeko kubwa la Wanyama hao.

Pia amewakaribisha wageni wote nchini na nje ya mipaka ya Tanzania kutembelea eneo hilo kwa kuwa ni eneo la kipekee lililobahatika kuwa na mnyama adimu anayeitwa choroa "Oryx".

Na Beatus Maganja- Makuyuni Wildlife Park

Chapisha Maoni

0 Maoni