Tanzania imeendelea kuaminiwa na kupewa nafasi ya kuandaa
mashindano ya tamasha la watu wenye usikivu hafifu (viziwi) la 2024 ambalo
linatarajiwa kufanyika katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambayo ni hifadhi
Bora Zaidi Barani Afrika.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe.
Dkt. Damas Ndumbaro usiku wa kuamkia Novemba 26, 2023 jijini Dar es Salaam
wakati akihitimisha tamasha hilo ambalo limefanyika kwa mara ya pili nchini
Tanzania.
“Serikali ya Tanzania inawakaribisha kwa mara nyingine tena,
Tanzania ni nchi ya amani na yenye vivutio vingi vya utalii, tamasha lijalo
litafanyika katika hifadhi yetu ya Taifa ya Serengeti ambayo imeshinda kuwa
hifadhi Bora zaidi Barani Afrika kwa mara ya Tano mfululizo. Nchi yetu
inathamini haki za watu wote na makundi yote, ulemavu sio mwisho wa maisha,
tutaendelea kushirikiana nanyi wakati wote,” amesema Dkt. Ndumbaro.
Katika mashindano hayo, Nashua Patience kutoka Uganda
ameibuka mshindi wa kwanza na kutwaa taji la mrembo kwa mwaka 2023 huku nafasi ya
mtanashati katika mashindano hayo ikinyakuliwa na Ariko David kutoka Uganda
wakati Mtanzania Caroline Mwakasaka akiibuka mshindi wa nafasi ya pili kwa
upande wa shindano la Mwanamitindo Bora "modal".
Kufanyika kwa mashindano hayo kwa mara ya pili mfululizo
nchini Tanzania ni fursa kwa jamii hiyo kujitangaza kwa watu wote duniani bila
kujali changamoto walizonazo pamoja na kutangaza vivutio vya Tanzania kupitia
jamii ya viziwi kote duniani.
Akimkaribisha Waziri Dkt. Ndumbaro, Katibu Mkuu wa Wizara
hiyo, Bw. Gerson Msigwa amesema Tanzania ipo tayari kuendelea kupokea
mashindano hayo mwaka 2024 akisisitiza kuwa Tanzania ni nchi ya upendo, utulivu
na amani huku akibainisha kuwa kupitia Tamasha hilo Watanzania wamenufaika na
kujifunza mambo mengi yaliyooneshwa na jamii hiyo kupitia ubunifu, vipaji,
umoja na Mawasiliano kupitia lugha ya alama.
Naye Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira
na Wenye Ulemavu) Mhe. Patrobas Katambi. amesema Serikali imeunda wizara
mahususi ili kusimamia watu wenye ulemavu na kujenga vyuo vya ufundi kwa watu
wenye ulemavu ili kuwapa ujuzi utakaowasaidia katika maisha yao.
Amesema Serikali inayoongozwa na Dkt.Samia Suluhu Hassan
imefufua vyuo vya watu wenye ulemavu kwa gharama ya shilingi billion 3.4,
imetoa fedha kiasi cha Sh. Bilioni 3 ili kujenga vyuo vipya vya ufundi vya watu
wenye ulemavu kwa lengo la kupata elimu, ujuzi na mafunzo stadi.
Aidha, amesema kila mwaka Serikali inatenga kiasi cha zaidi
ya milioni 60 kwa ajili mafuta kwa watu wenye changamoto ya ngozi pamoja na
kututoa fedha za kukarabati mabweni katika halmashauri 50 nchini kwa gharama ya
Sh. Bilioni 4 ili watu wenye ulemavu wapate haki na stahiki zao.
Naye rais wa Chama cha Viziwi Afrika na Tanzania Habibu
Mrope pamoja na Bi. Bonita Ann Leek Mkurugenzi
wa Miss na Mr Deaf International (MMDI) wameishukuru Tanzania ambayo inaongozwa
na Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kuwa wenyeji wa mashindano hayo kwa
mara ya pili hatua inayowatia nguvu na hamasa watu wenye usikivu hafifu.
Tamasha hilo limehusisha washiri zaidi ya 200 kutoka mataifa
ya Afrika Kusini, Australia, Belarus, Brazil, Ethiopia, Falme za Kiarabu,
Guyana, Haiti, Hispania, India, Iran, Italia, Kenya, Kongo DRC, Malasia,
Macedonia, Marekani, Mexico, Misri, Morocco, Msumbiji, Nigeria, Pakistan,
Poland, Romania, Rwanda, Senegal, Siera Leone, Sudan Kusini, Thailand, Tunisia,
Jamhuri ya Czechoslovakia, Ufaransa, Uganda, Ujerumani, Ukraine, Urusi, Zambia,
Zimbabwe na wenyeji Tanzania.
Na Eleuteri Mangi- WUSM
0 Maoni