Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Kamishna
Benedict Wakulyamba ameeleza kuridhishwa kwake na Kasi ya utendaji mzuri wa
Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA katika kulinda rasilimali
za nchi bila kujali vipingamizi vinavyo jitokeza katika utekelezaji wa majukumu
hayo ya kitaifa.
Ameyasema hayo wakati wa ziara yake Makao Makuu ya ofisi za
TAWA Mkoani Morogoro alipokuwa akiongea na Menejimenti ya Taasisi hiyo jana ikiwa
ni ziara yake ya kwanza tangu alipoteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dr Samia Suluhu Hassan kushika nafasi ya Naibu Katibu Mkuu.
"Niwapongeze kwa kazi kubwa mnayoifanya, kazi nzuri
sana sana mnayoifanya achilia mbali changamoto mbalimbali lakini kiukweli kazi
mnaifanya," amesema Kamishna Wakulyambia.
Kamishna Wakulyamba amesema lengo la kwanza la kuanzishwa
kwa Taasisi za uhifadhi nchini hususan Taasisi za kijeshi za uhifadhi, ni
kuimarisha ulinzi wa maliasili hivyo kwa niaba ya Wizara ya Maliasili na Utalii
amezielekeza Taasisi hizo kuimarisha ulinzi wa rasilimali za nchi kwa nguvu
zote ili ziweze kutumika kwa manufaa na lengo la utalii.
"Lazima tulinde maliasili zetu kwa udi na uvumba, ndiyo
kazi tuliyokabidhiwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba, hatujapewa
kwa hisani ya mtu tumepewa kwa mujibu wa Katiba na sheria za bunge la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, " amesisitiza Kamishna Wakulyamba
Pia amesisitiza kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii ni Wizara
ya kibiashara na kimkakati hivyo Mamlaka inapaswa kujidhatiti katika kuimarisha
vitengo vya utalii na masoko kwa lengo la kuiingizia Serikali mapato.
Awali akiwasilisha taarifa ya utendaji wa TAWA kwa Mwaka
2022/23 kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA Mabula Misungwi Nyanda,
Kamishna Msaidizi Mwandamizi Asha Kilili amesema mojawapo ya mafanikio ya TAWA
kwa Mwaka huo wa fedha ni kutoa elimu na mbinu rafiki za kujikinga na madhara
yanayosababishwa na Wanyamapori Wakali na Waharibifu kwa wananchi zaidi ya Laki
nne katika jumla ya vijiji 1,319 ikiwa ni pamoja na kukamilisha ujenzi wa vituo
16 vya askari wa kudhibiti wanyama hao na kuweka vitendea kazi ikiwemo pikipiki
50.
Sambamba na hilo Asha Kilili amesema TAWA iliweza kufukuza
jumla ya tembo takribani 554 kwa helkopta katika wilaya za Nachingwea, Liwale,
Same na Bunda ikiwa ni pamoja na kufunga visukuma mawimbi kwa viongozi wa
makundi ya tembo 8 katika wilaya za Same, Tunduru, Liwale na Nachingwea.
Aidha amesisitiza kuwa TAWA itaendelea kuongeza ubunifu na
mbinu mbalimbali katika kukabiliana na matukio ya Wanyamapori Wakali na
Waharibifu, ulinzi wa rasilimali za Wanyamapori pamoja na kuongeza mapato.
Na. Beatus Maganja- Morogoro
0 Maoni