Serikali ya awamu ya sita
kupitia Wizara ya Afya imesema kuwa itahikikisha kuwa inaboresha upatikanaji wa
huduma bora za afya kwa wote kupitia mfumo wa bima ya afya kwa kuweka mfumo wa
ushiriki katika skimu za bima ya afya kwa raia na wakazi wake wote.
Kauli hiyo imetolewa Bungeni
jana na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu wakati akiwasilisha muswada wa kutunga
sheria ya bima ya afya kwa wote ambapo ameeleza kuwa lengo la kuanzishwa kwa
muswada huo wa Bima ya Afya kwa wote ni kutimiza wajibu wa Serikali wa kikatiba
wa kuhakikisha kuwa wananchi wote wanapata huduma bora za afya bila kikwazo.
Mhe. Ummy amesema kuwa
utaratibu wa kawaida wa kuchangia gharama za matibabu unachangamoto nyingi
ikiwa ni pamoja na wananchi wengi kukosa huduma za afya kutokana na kukosa
fedha za kugharamia matibabu papo kwa papo jambo ambalo linawapelekea wananchi
kuingia katika janga la umasikini.
“Tunayo mifano iliyo hai ya
wananchi ambao walilazimika kuuza mali zao ikiwemo mashamba, mifugo, vyombo vya
usafiri, vifaa vya ndani na kuweka rehani mali zao ili kugharamia matibabu yao
au ya wapendwa wao,” amesema Mhe. Ummy.
Mhe. Ummy amesema dhana ya
huduma za afya kwa wote imejengeka katika nguzo kuu tatu ambazo ni uwezo wa
kuwafikishia wananchi huduma za afya, upatikanaji wa huduma bora za afya na
mfumo madhubuti wa ugharamiaji wa huduma za afya bila kikwazo cha fedha hivyo
ni wakati sasa wa kila mwananchi kujiunga na bima ya afya kwa wote.
Akizungumzia upatikanaji wa
bima kwa watu wasio na uwezo ameeleza kuwa Serikali ya awamu ya sita
itahakikisha kuwa watu wasio na uwezo wanapata huduma bora za afya kwa kuweka
mfumo maalumu ambao utagharamia bima ya afya kwa watu wa hali ya chini.
Pia ameongeza kuwa ni wajibu
wa Serikali kuhakikisha wananchi wasio na uwezo wanapata huduma bora za afya na
katika kuwatambua watu wasio na uwezo mapendekezo ya Serikali ni kuboresha
mifumo ya utambuzi wa watu kwa kutumia Mamlaka zilizopo za takwimu za utafiti
wa mapato ili kuwaweka katika utaratibu wa bima ya afya.
0 Maoni