Hospitali ya Taifa Muhimbili imefanya upasuaji wa kuondoa
mtoto wa jicho kupitia njia ya kisasa ya matundu madogo (Phacoemulsification)
ambapo katika hospitali za umma nchini inakua ya kwanza kufanya upasuaji wa ina
hii.
Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji, Dkt. Rachel Mhaville
amesema upasuaji huu umeenda sambamba na mafunzo ya kuwajengea uwezo wataalamu
wa ndani pamoja na hospitali zingine kwa lengo la kuwezesha huduma hii
kuwafikia Watanzania wengi zaidi umefanywa na wataalamu wa MNH kwa kushirikiana
na wataalamu kutoka Korea na kupitia Taasisi ya Vision Care Tanzania.
Amesema MNH inapambana kutoa huduma za kibingwa na bobezi
kwa Watanzania na nchi jirani ili kuhakikisha kama Hospitali ya Rufaa ya Taifa
inakua kitovu cha utalii tiba.
‘‘Muhimbili inaendelea kunyoosha njia chini ya uongozi wa
Mkurugenzi Mtendaji Prof. Mohamed Janabi na kuishi ndoto ya Mh. Rais Dkt. Samia
Suluhu Hassan ya kuhamasisha utalii tiba nchini na kufikia kile ambacho
tunataka kufikia kama nchi,’’ amefafanua Dkt. Mhaville.
Akielezea kuhusu upasuaji huo, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya
Macho Muhimbili Joachim Kilemile amesema upasuaji huu ni tofauti na uliokuwa
unatumika awali ambapo mgonjwa alikuwa anapasuliwa sehemu kubwa ili kuweza
kutoa mtoto wa jicho.
Kwa mujibu wa Dkt. Kilemile upasuaji huu una faida nyingi
kwakuwa mgonjwa anapona kwa muda mfupi na kuendelea na shughuli zake kama
kawaida ambapo takribani wagonjwa 50 watanufaika na huduma hiyo.
‘‘Sababu za mtu kupata mtoto wa jicho ni umri kubwa,
magonjwa mbalimbali ikiwemo ugonjwa Kisukari kwa wale wenye umri mdogo hasa
pale ugonjwa huo usipodhibitiwa vizuri, magonjwa ya figo na Ngozi,’’ ameeleza
Dkt. Kilemile.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Taasisi ya Vision Care
Tanzania Bi. Jieun Park amesema Vison Care itaendelea kushirikina na Muhimbili
kuwajengea uwezo wataalamu na kusaidia upatikanaji wa vifaa tiba ili kuendelea
kuboresha huduma za macho Muhimbili.
0 Maoni