Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imekabidhiwa
tuzo ya ushindi wa kwanza kwa upande wa kundi la Wizara iliyofanya vizuri
katika kutekeleza uwezeshaji wananchi kiuchumi.
Tuzo hiyo iliyotolewa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji
Wananchi Kiuchumi (NEEC) imekabidhiwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa kwa
Waziri wa Ardhi Mhe. Jerry Silaa wakati wa ufungaji Kongamano la Saba la
Uwezeshaji Kiuchumi katika ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.
Akizungumza kwenye kongamano hilo, Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa
amewataka Viongozi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma na Sekta Binafsi
kuimarisha huduma za uwezeshaji ili kufikia malengo waliojiwekea na kutimiza
dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kukuza uwezeshaji na kupunguza
umaskini nchini.
ametoa miezi mitatu kwa Wakuu wa Mikoa yote nchini ambao
bado hawajaanzisha vituo vya uwezeshaji wananchi kiuchumi kama ilivyoelekezwa
katika Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020/2025 wawe wameshaanzisha kabla ya mwaka
2024.
Awali, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji
Wananchi Kiuchumi (NEEC), Beng'i Issa alisema kongamano hilo linalenga kuongeza
ufahamu wa wadau mbalimbali kuhusu dhana ya uwezeshaji wananchi kiuchumi na
kuwakumbusha majukumu waliyonayo katika kuwawezesha Watanzania.
Alisema malengo mengine ni pamoja na wadau kupeana uzoefu
katika kutekeleza shughuli za uwezeshaji wananchi kiuchumi, kuzindua taarifa ya
mwaka 2022/2023 ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi
ya mwaka 2004 ambayo pia imejumuisha masuala ya ushiriki wa Watanzania katika
miradi ya kimkakati na uwekezaji unaofanyika nchini.
0 Maoni