Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro
ameiagiza Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) iandae taarifa kuhusu mgogoro
wa Hakimiliki kwa kazi ya ubunifu wa michoro ya Tingatinga pamoja na kufuatilia
Mtunzi na Mmiliki wa Wimbo wa "Malaika Nakupenda" kwa kushirikiana na
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa kuwa Wimbo huo ni maarufu duniani na
umekuwa ukirudiwa kuimbwa na watu mbalimbali.
Dkt. Ndumbaro ametoa agizo hilo jana Jijini Dar es Salaam
alipotembelea Ofisi ya COSOTA ikiwa ni ziara yake ya kwanza iliyolenga kufahamu
majukumu ya Taasisi hiyo.
"Ubunifu ni kitu cha msingi sana katika maendeleo ya
Taifa hivyo usimamizi wa Hakimiliki kwa kazi hizi za ubunifu ni muhimu. Tanzania
tumeridhia kuwa sehemu ya Soko Huru la Afrika (African Continental Free Trade
Area -AfCFTA) na kazi za sanaa, uandishi na ubunifu wa watu wetu zitasambaa kwa
kasi hivyo ni vyema tujipange katika kuzilinda kazi hizi, tuzisajili kwa wingi
ili tusiibiwe," amesisitiza Dkt. Ndumbaro.
Ameeleza kuwa, baadhi ya kazi za Wasanii zimekuwa zikitumika
katika mataifa mbalimbali duniani na kuleta mgogoro katika utambulisho wa
Hakimiliki, pia mapato mengi ya Wabunifu wa kazi hizo yamekuwa yakipotea
akibainisha kuwa kuna wadau kama Tingatinga ambao hawawezi kupambania haki yao
wenyewe bila Serikali kuwasaidia.
Pia ameiagiza COSOTA ifanye Operesheni ya kupambana na
Uharamia wa kazi za ubunifu katika maeneo mbalimbali nchini na pia itenge
bajeti itakayowezesha Maafisa kuwafuata wadau ili kusajili kazi zao.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu na Msimamizi wa Hakimiliki nchini,
Doreen Sinare amesema marekebisho yaliyofanyika katika Sheria ya Hakimiliki na
Hakishiriki kuanzia mwaka 2019, 2022 na 2023 yameiwezesha Tanzania ianze
kunufaika baada ya Bunge Kuridhia Mkataba wa Marrakesh ambapo Shirika la Miliki
Bunifu Duniani (WIPO) lilileta mradi wa kuandaa vitabu na tayari limeshatoa
msaada wa vifaa kwa Chama cha Wasioona Tanzania vinavyoweza kutumika shuleni na
vinatarajiwa kusambazwa katika Shule 7 nchini.
"COSOTA tumepokea maelekezo yote na tunaahidi
kuyafanyia kazi kwa wakati," Bi. Doreen.
0 Maoni