Ikiwa ni Jitihada za Serikali kuendelea kuweka mazingira
rafiki ya kiuwekezaji katika Sekta ya Madini nchini, Wizara ya Madini na Chemba
ya Migodi zimekutana, ikiwa ni mwendelezo wa utaratibu uliowekwa na Wizara
kukutana na Wachimbaji Wakubwa, wa Kati na Watoa huduma migodini kila Robo ya
Mwaka kupitia Chemba ya Migodi.
Mkutano huo ni wa pili kufanyika baada ya mkutano wa kwanza
uliofanyika mapema mwezi Julai, 2023, yote ikilenga kuleta ukaribu kati ya
serikali na wadau wa sekta ya madini pamoja na kujadili kwa pamoja changamoto
ili kuondoa vikwazo mbalimbali vinavyozuia utekelezaji wa miradi, shughuli na
biashara ya madini nchini.
Akizungumza katika mahojiano maalum, Waziri wa Madini Mhe.
Anthony Mavunde ambaye amekutana na wadau hao kwa mara ya kwanza tangu
kuteuliwa na kuapishwa kuwa Waziri wa Madini, amesema, mikutano hiyo inatumika
kama njia ya kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili katika utekelezaji
wa miradi wanayoisimamia ili kuchochea uwekezaji.
‘’Tukiondoa vikwazo itasaidia kuongeza shughuli za uchimbaji
nchini na hatimaye tutaongeza uchumi na mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato
la Taifa, tutaongeza ajira, maendeleo ya nchi na watu. Chukulia mfano wa Mkoa
wa Geita tu, Serikali inakusanya shilingi bilioni 243, tunataka shughuli za
madini zifanyike mikoa yote katika mazingira rafiki,’’ amesisitiza Mavunde.
Katika hatua nyingine, Mhe. Mavunde amefungua mlango kwa
wawekezaji wote nchini na kueleza kuwa hategemei kuwa kikwazo kwao na kuwataka
kuendelea kushirikiana na Serikali kuendeleza Sekta ya Madini nchini.
‘’ Kwenye ufunguzi wa Mkutano wa Tano wa Uwekezaji Sekta ya
Madini nilisema moja ya vitu nisivyovipenda ni urasimu. Nipo hapa kuondoa
urasimu nitafanya kazi na ninyi na tutashirikiana vizuri, ‘’ amesema Waziri
Mavunde.
Aidha, ametumia jukwaa hilo kuwapongeza na kuwashukuru wadau
hao na kueleza kuwa, kwa pamoja wamewezesha kuongeza mchango wa Sekta ya Madini
kwenye Pato la Taifa kufikia asilimia 9.1 katika Mwaka wa Fedha 2022/23.
Waziri Mavunde ameendelea kuwasisitiza kuhusu dhamira ya
Serikali kutekeleza Vision *2030: Madini ni Maisha na Utajiri* ambapo amesema
Wizara kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti Tanzania (GST) inalenga kufanya
tafiti za kina kwa kutumia ndege ili kufikia asilimia 50 ifikapo mwaka 2030 kutoka
asilimia 16 ya sasa. Tunatakakwenda kwenye uchumi wa madini mkakati. Tanzania
ina utajiri wa kutosha wa madini mkakati na kwa kuzingatia mahitaji ya dunia ya
tani milioni 150 ya madini hayo ifikapo mwaka 2050 ni lazima ijipange kunufaika
ipasavyo kiuchumi,’’ amesema Mhe. Mavunde.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chemba ya Migodi Mhandisi
Philbert Rweyemamu amesema kuwa lengo la mikutano hiyo ni kujadili na kujenga
uelewa wa pamoja katika masuala mbalimbali hususan masuala yanayohusu mifumo ya
Kisheria na Kisera na kuongeza kwamba, mikutano hiyo inalenga kuiwezesha sekta
ya madini kuendelea kufanya vizuri.
Awali, Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali amesema
utaratibu huu unawezesha serikali kupata mrejesho na kufanyia kazi changamoto
mbalimbali zinazowasilishwa na wadau na kueleza kuwa, lengo la serikali ni
kuwawezesha wadau kutekeleza majukumu yao vizuri kupata faida na serikali
kunufaika kupitia rasilimali madini.
‘’Tayari Wizara imeweka utaratibu kuwa na focal point katika
kila miradi inayotekelezwa ili kuwawezesha wadau kufanya kazi zao kwa muda
uliopangwa na serikali kupata mrejesho wa haraka,’’ amesisitiza Mahimbali.
Aidha, katika mkutano
huo, Wizara imetoa mrejesho wa yale yaliyojadiliwa katika mkutano uliopita.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wadau hao wamepongeza
utaratibu wa kukutana na kujadili kwa pamoja na baadhi kupendekeza taasisi
nyingine za umma zinazohusika na masuala ya madini moja kwamoja kushirikishwa
katika mikutano hiyo ili kuendelea kuweka mazingira wezeshi katika sekta ya
madini.
Mbali na wanachama wa Chemba ya Migodi, mkutano huo
umehudhuriwa na watendaji wa taasisi zilizo chini ya wizara na wawakilishi
kutoka Ubalozi wa Australia.
Na. Wizara ya Madini- Dar es Salaam
0 Maoni