Tanzania imefanikiwa kudhibiti vitendo vya ukeketaji kwa
watoto wa kike 245 kupitia mpaka wa Tanzania na Kenya kwa mkoa wa Mara katika
msimu wa ukeketaji mwaka jana.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima wakati wa mdahalo kuhusu
jitihada zinazofanywa na nchi wanachama wa Umoja wa Afrika katika kutokomeza
vitendo vya ukeketaji unaovuka mipaka ikiwa ni sehemu ya Mkutano wa Kimataifa
wa masuala ya Ukeketaji unaoendelea katika ukumbi wa JNICC jijini Dar es Salaam.
Katika mjadala huo ambapo washiriki wamepeana uzoefu wa
jinsi ya kudhibiti watoto wasiende kukeketwa nje ya mipaka wakati wa misimu ya
ukeketaji, Waziri Dkt. Gwajima amesema Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na
Taasisi mbalimbali za Umma na binafsi liliwakamata watu zaidi ya 20 waliohusika
na vitendo hivyo na baada ya zoezi hilo, Tanzania imeendelea kutoa elimu kwenye
jamii kupitia vyombo mbalimbali vya Habari.
"Lakini haitoshi kusubiri msimu wa ukeketeji watoto
wanakimbia wanavushwa mipaka ni lazima tujikite ndani kwenye jamii zetu ambapo
Tanzania tumeshatengeneza Mkakati wa Kutokomeza Ukeketaji pamoja na Mpango kazi
wake wa utekelezaji wa mwaka 2021 -2025" amesema Waziri Dkt. Gwajima.
Ameeleza kwamba mkakati huo utahusisha elimu na huduma kwa
manusura wa ukeketaji pamoja na kufikia hadi ngazi ya vijiji kwa sababu ni
suala la ukeketaji limekuwa sio tu mila na desturi bali kwenye imani, uchumi na
siasa.
"Jamii haiangalii tena madhara yanayotokana na
ukeketaji kwa watoto wetu, suala hili limekuwa kama imani na kutumiwa na baadhi
ya wanasiasa pia hivyo elimu kwa viongozi pia muhimu," ameongeza Waziri
Gwajima.
Wengine walioshiriki mdahalo huo ni Waziri wa Jinsia, Kazi
na Maendeleo ya Jamii, kutoka Uganda, Mituuzo Peace Regis, Afisa Mtendaji Mkuu
wa Masuala ya ukeketaji kutoka Kenya Bernadetha Loloju na Mkurugenzi wa masuala
la Wanawake kutoka Ethiopia Seleshi Tadesse.
Na. WMJJWM- Dar es Salaam
0 Maoni