Wataalamu wa magonjwa ya moyo na mfumo wa umeme wa moyo wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wanapewa mafunzo kwa vitendo ya jinsi ya
kuwahudumia wagonjwa wenye matatizo sugu ya hitilafu katika msukumo wa damu na
utengenezaji wa mapigo ya moyo.
Mafunzo hayo ya siku tatu yanatolewa na Prof. Antonio Curnis
ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Magonjwa ya Moyo na daktari bingwa wa magonjwa
ya moyo na mfumo wa umeme wa moyo kutoka chuo kikuu cha Brescia kilichopo nchni
Italia.
Prof. Curnis alisema lengo la mafunzo hayo ni kubadilishana
ujuzi wa kazi wa jinsi ya kuwahudumia wagonjwa wenye matatizo ya moyo kushindwa
kufanya kazi, wenye matatizo sugu ya hitilafu katika msukumo wa damu na
utengenezaji wa mapigo ya moyo pamoja na kufundisha teknolojia mpya ya jinsi ya
kutoa matibabu hayo.
“Wagonjwa wenye matatizo ya moyo kushindwa kufanya kazi kama
watatibiwa mapema na vizuri wanaweza kuishi muda mrefu zaidi ya miaka 10 na
hivyo kuokoa gharama za matibabu yao, lakini kama watachelewa kupata matibabu
na hawatapata matibabu mazuri muda wao wa kuishi huwa ni mfupi,” alisema Prof.
Curnis.
“Mimi na wenzangu tumekuja Tanzania kutoa mafunzo haya kwa
wataalamu wa hapa nchini ili wagonjwa wenye matatizo ya moyo kushindwa kufanya
kazi na wenye matatizo sugu ya hitilafu katika msukumo wa damu na utengenezaji
wa mapigo ya moyo waweze kupata matibabu mapema na kwa wakati,” alisema Prof.
Curnis.
Alizitaja sababu za moyo kushindwa kufanya kazi kuwa ni
pamoja na mishipa ya damu ya moyo kuziba, msongo wa mawazo, shinikizo la juu la
damu, kisukari, unywaji wa pombe kupita kiasi na matatizo ya ujauzito na dalili
zake ni mgonjwa kushindwa kupumua na mapigo ya moyo kupungua tofauti na
inavyotakiwa kuwa.
Akizungumza kuhusu mafunzo hayo daktari bingwa wa magonjwa
ya moyo na mfumo wa umeme wa moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Yona
Gandye alisema mafunzo hayo yatawasaidia kupata ujuzi wa jinsi ya kutoa huduma
kwa wagonjwa wenye matatizo sugu ya hitilafu ya mfumo wa umeme wa moyo na wenye
matatizo ya moyo kushindwa kufanya kazi.
“Mafunzo haya yatatuwawezesha wataalamu wa JKCI na wenzetu
wa nchini Italia kushirikiana kwa pamoja na kubadilishana uzoefu wa kutoa
matibabu kwa wagonjwa wenye matatizo sugu ya hitilafu ya mapigo ya moyo na moyo
kushindwa kufanya kazi”, alisema Dkt. Gandye.
Dkt. Gandye alisema licha ya mafunzo hayo kufanyika kwa njia
ya vitendo pia yanatoa nafasi kwa wagonjwa sita kupata huduma ya matibabu itakayowasaidia
kupandisha mapigo ya moyo na kuwezesha mioyo yao kufanya kazi vizuri kwa
kupandikizwa vifaa visaidizi vya moyo ambavyo ni Pacemaker na Cardiac
Resynchronization Therapy Device - CRTD.
Mafunzo hayo yanafanyika kwa ushirikiano wa JKCI, Kas Medics
Limited, Abbott na Chama cha madaktari katika tiba ya hitilafu ya mapigo ya
moyo (Device and Arrhythmic Society of Tanzania – DAR Tanzania) ambao
walichagua wataalamu kutoka hospitali inayotibu wagonjwa wenye matatizo sugu ya
hitilafu katika msukumo wa damu na utengenezaji wa mapigo ya moyo ili waweze
kutoa mafunzo hayo kwa wataalamu wa hapa nchini.
Katika mafunzo hayo Abbott na Kas Medics Limited wametoa
msaada wa vifaa tiba ambavyo ni Pacemaker na Curiously Recurring Template
Pattern (CRTP) vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 60.
Mafunzo hayo yanakwenda sambamba na kongamano la siku moja
litakalofanyika leo tarehe 31 Oktoba jijini Dar es Salaam litakalokuwa na mada
za moyo kushindwa kufanya kazi na mapigo ya chini ya moyo ambalo limewalenga madaktari
wote Tanzania hususani wanaohusika na utoaji wa tiba ya moyo ili waweze kutoa
huduma za matibabu hayo pindi watakapokutana na wagonjwa wa aina hiyo.
0 Maoni