Serikali kupitia Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA)
inaendelea na zoezi la uandikishaji wa wananchi wa Tarafa ya Ngorongoro ambao
wameunga mkono jitihada za Serikali kuboresha maisha yao ambayo kwa miaka mingi
wamekosa fursa mbalimbali za kimaendeleo kwa kuishi ndani ya eneo la Hifadhi ya
Ngorongoro.
Kwa mujibu wa Kamishna Msaidizi Mwandamizi Mdala Edson Fedes
ambae ni meneja mradi huo amebainisha kuwa katika awamu ya kwanza ya
utekelezaji wa zoezi hilo jumla ya kaya 551 zenye watu 3,010 na mifugo 15,321
ziliandikishwa, kuthaminishwa na kuhamishwa ndani ya Hifadhi.
Aidha, katika awamu ya pili ya utekelezaji wa zoezi hili,
ndani ya muda mfupi baada ya wananchi kusikia Serikali imeanza ujenzi wa nyumba
5,000 kwa ajili ya wananchi hao, hadi kufikia tarehe 10 Oktoba, 2023 tayari
kaya 434 zimeshajiandikisha.
Zoezi la kutoa elimu, kuandikisha na kuthaminisha kaya
zilizopo tayari kuhama linaendelea na idadi inaataarajiwa kuongezeka kwa kasi kutokana
na muamko wa wananchi kuunga mkono jitihada za Serikali zinazoendelea katika
kuboreshaa maisha yao.
Kamishna Fedes ameongeza kuwa wakati kazi ya ujenzi wa
nyumba 5,000 katika maeneo ya Msomera - Handeni, Saunyi - Kilindi, Kitwai
Simanjiro ukiendelea, kuanzia wiki ijayo Serikali itahamisha kaya ambazo
zimejiandikisha na ziko tayari kuhamia maeneo ambayo wameyachagua wenyewe.
Tayari Serikali kupitia SUMA-JKT mapema mwezi oktoba, 2023
imeanza utekelezaji wa mradi wa kujenga nyumba 5,000 kwa ajili ya wananchi
wanaojiandikisha kuhama kwa hiari na ujenzi wa nyumba hizo unatarajiwa
kukamilika mwishoni mwa mwezi Machi, 2024.
Wananchi wanaojiaandikisha kuhama kwa hiari wanapata fursa
ya kufidiwa mali zao, kupewa nyumba yenye eneo la ekari 2.5, kupatiwa shamba la
ekari 5 kwa ajili ya kilimo, huduma muhimu za kijamii kama vituo vya afya,
shule, maji, umeme, barabara, mawasiliano, vituo vya polisi, posta na
miundombinu ya mifugo kama malisho, josho, malambo na huduma nyinginezo.
Na. Kassim Nyaki- NCAA
0 Maoni