WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ametoa wito kwa viongozi wa
dini kuwahimiza vijana kufanya kazi kwa staha, weledi na uadilifu ili kuzitumia
rasilimali zilizopo nchini kujiletea maendeleo.
Nchi yetu imebarikiwa fursa nyingi za kiuchumi, ili jamii
ione matunda ya uwepo wa fursa hizo tunategemea sana nguvu kazi ya vijana
katika kuzitumia rasilimali zilizopo”
Majaliwa ametoa wito huo leo Jumapili (Oktoba 01, 2023)
wakati wa Jubilei ya miaka 125 ya Uinjilishaji katika Jimbo Kuu Katoliki la
Songea, kwenye kilima cha Peramiho, Songea mkoani Ruvuma.
Aidha, amezisihi Taasisi za dini kuweka mipango mahsusi na
shirikishi ya malezi ya vijana. “Tumieni nafasi zenu kuongeza msukumo wa malezi
kwa vijana kwa kuweka mifumo ya kuwafuatilia kwa karibu na kuhimiza ushiriki
wao kwenye vyama vya kitume”
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amewasihi viongozi wa dini
waendelee kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa masuala ya kipaumbele
yanayohusu ustawi wa Taifa.
“Niwasihi sana mtuunge mkono kuhamasisha uhifadhi wa
mzingira na matumizi ya nishati safi, kampeni za kupanda miti na usafi wa
mazingira, kukemea vikali vitendo vya mmomonyoko wa maadili, matumizi ya madawa
ya kulevya na kukemea vitendo vya rushwa,” alisema Majaliwa.
Katika Hatua nyingine, Waziri Mkuu ameyapongeza madhehebu ya
dini kwa kuendelea kutoa huduma mbalimbali za kijamii kwenye sekta za elimu,
afya, maji na huduma nyingine za kijamii hasa katika maeneo ya pembezoni.
“Kazi hiyo
mnayoifanya ya kutoa huduma kwa jamii ni kuunga mkono dhamira ya Mheshimiwa
Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuboresha
ustawi wa jamii ya Watanzania kwa kusogeza huduma zote muhimu karibu na
wananchi,” alisema Majaliwa.
Katika Jubilei hiyo, Rais Dkt. Samia ametoa shilingi milioni
kumi kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 125 ya Jubilei ya Uinjilishaji katika
jimbo Kuu Katoliki la Songea.
Naye, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Songea Damian
Dallu ameishukuru Serikali kwa ushirikiano inaoutoa katika shughuli mbalimbali
za huduma za jamii na uinjilishaji zinazofanywa na kanisa katoliki nchini.
CHANZO: Ofisi ya Waziri Mkuu
0 Maoni