Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajia kufanya ziara ya Kitaifa nchini India kuanzia tarehe 8 hadi 11 Oktoba 2023 kufuatia mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya India, Mheshimiwa Droupadi Murmu.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Mhe. January Makamba (Mb) amewaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salam
kuwa ziara hiyo inafanyika ikiwa ni miaka minane imepita tangu ziara ya mwisho
ya Kiongozi wa Tanzania nchini humo iliyofanywa na Rais wa Awamu ya Nne, Mhe.
Jakaya Mrisho Kikwete mwaka 2015.
Akiongelea umuhimu wa ziara hiyo, Mhe. Waziri Makamba
amesema ziara hiyo ni muhimu kutokana na historia iliyopo kati ya Tanzania na
India kidiplomasia, kiuchumi, kibiashara, kidini, kiutamaduni na Maisha ya
India ambayo yapo nchini Tanzania.
Amesema ziara hiyo ina lenga kuendeleza ushirikiano kati ya
Tanzania na India na kuongeza kuwa katika ziara hiyo makubaliano ya
kushirikiana kupitia sekta za kimkakati kama afya, viwanda, ulinzi na usalama,
elimu, teknolojia ya habari na mawasiliano, uchumi wa buluu, maji, kilimo,
biashara na uwekezaji pamoja na kutangaza fursa za biashara na uwekezaji za
Tanzania ili kuvutia wawekezaji na wafanyabiashara wa India waje nchini.
Akiongelea faida zinazotarajiwa kupatikana kutokana na ziara
hiyo, Mhe. Makamba amesema katika ziara hiyo inatarajiwa kuwa hati mbalimbali
za makubaliano zitasainiwa na hivyo kuleta tija katika maeneo ya Mafunzo ambapo
Maelfu ya Watanzania watapata nafasi za mafunzo na kujengewa uwezo katika
nyanja mbalimbali nhini India na kuongeza kuwa India imeazimia kutoa ufadhili
na fursa za mafunzo zaidi ya elfu moja katika fani mbalimbali.
Amesema ziara hiyo itawezesha maendeleo na mapinduzi ya
kidijitali na inatarajiwa kuwa India itaanzisha kiwanda cha mitambo ya kuunda
bidhaa za kielektroniki na kuanzisha mifumo ya kutumia Akili Tarakilishi
nchini.
Amesema kuwa ziara hiyo inatarajia kuinua ubora wa huduma za
Afya nchini ambapo taasisi ya upandikizaji wa figo na kiwanda cha kutengeneza
chanjo za wanyama na binadamu zenye ubora vitaanzishwa, kuwezesha ushirikiano
mkubwa kati ya Hospitali zetu na Hospitali za India zinazotoa huduma za afya
kwa mifumo ya Tiba Asilia pamoja na kuwezesha upatikanaji wa dawa zenye ubora kwa
gharama nafuu.
Akiongelea faida itakazopata sekta ya Kilimo Mhe Waziri
Makamba amesema kupata masoko kwa mazao ya kilimo kwa kuwa tunazalisha mbaazi,
korosho na mazao mengine ambayo India ni sehemu ya soko pamoja na kuinua na
kuongeza biashara ya mazao yanayozalishwa nchini hususan mbaazi, kunde,
parachichi na ufuta.
“Tukumbuke kuwa bei ya mbaazi mwaka huu imekuwa kubwa hii ni
kwa sababu India wamenunua mbaazi kwa wingi kwahiyo ziara hii itahakikisha soko
la mbaazi linakuwa kubwa na linaendelea kuwepo sio msimu huu lipo au msimu
ufuatao linakosekana,” alisema Mhe. Waziri.
Amesema ziara hii pia itawezesha uwekezaji wa moja kwa moja
kwa kuvutia uwekezaji kutoka kwa wafanyabiashara wakubwa na kampuni mbalimbali
kutoka India; kuimarisha Ulinzi na Usalama katika usafiri wa majini ambapo
India inatarajia kuanzisha karakana ya utengenezaji wa vyombo vya majini na
ukarabati.
Mhe. Waziri Makamba amesema katika ziara hiyo Mhe. Rais
Samia anatarajiwa kufungua Kongamano la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania
na India
litakalowezesha wafanyabiashara na kampuni mbalimbali za
nchini kupata fursa za kufanya biashara ya bidhaa zao na uwekezaji nchini India
na kushiriki mikutano ya uwili na majadiliano kati ya wafanyabiashara wa
Tanzania na wafanyabiashara wa India pamoja na kushuhudia ubadilishinaji wa
Hati za Makubaliano kati ya Sekta Binafsi za Tanzania na India.
Akiongelea kuhusu ushirikiano kati ya Tanzania na India,
Mhe. Waziri Makamba amesema Uhusiano huo uliasisiwa na waasisi wa mataifa hayo
Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Mahatma Gandhi
ulitokana na falsafa za viongozi hao ambao walipenda kutafuta suluhu ya amani
pasipokuwa na umwagaji damu.
Akiongelea yatakayojiri katika ziara hiyo Mhe. Waziri
Makamba amesema Mhe. Rais Samia akiwasili nchini India atapokelewa rasmi tarehe
9 Oktoba, 2023 na Rais wa India, Mhe. Droupadi Murmu ambaye ataambatana na Mhe.
Narendra Modi, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya India na kufanyiwa sherehe za mapokezi
rasmi ambayo yatahusisha gwaride rasmi na kupigiwa mizinga 21.
Baada ya mapokezi hayo, Mhe. Rais Samia atakuwa na
mazungumzo ya faragha na Mhe. Waziri Mkuu Modi na kufuatiwa na mazungumzo ya
uwili kati ya ujumbe wa Tanzania na India na watashuhudia ubadilishanaji wa
Mikataba na Hati za Makubaliano kati ya Tanzania na India na baadaye kuzungumza
na waandishi wa habari kuelezea muhtasari wa mazungumzo yao.
Jioni ya siku hiyo Mhe. Rais Samia atazungumza na mwenyeji
wake, Rais wa India, Mhe. Droupadi Murmu na kushiriki dhifa ya kitaifa
itakayoandaliwa kwa heshima yake na mwenyeji wake katika Ikulu ya India.
0 Maoni