Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof.
Mohamed Janabi ameishauri jamii kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza kwa kuweka
utaratibu mzuri wa kula na kufanya mazoezi mara kwa mara kuwa kuwa magonjwa
hayo yamekuwa tishio ambapo yanachangia idadi kubwa ya vifo vinavyotokea
ulimwenguni.
Prof. Janabi ameyasema hayo leo wakati akifungua mafunzo
maalum ya kutambua magonjwa ya moyo na namna ya kufanya vipimo vya moyo kwa
kutumia kifaa maalum kiitwacho Echocardiography.
Prof. Janabi ameongeza kuwa inakadiriwa watu milioni 17.9
wamefariki mwaka 2019 kutokana na magonjwa ya moyo ambapo asilimia 85 ya
magonjwa hayo yalitokana na mshtuko wa moyo uliopelekea kiharusi ambapo
yanaathri kwa kiasi kikubwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, Tanzania
ikiwemo.
“Ni vizuri tukafanya uchunguzi wa afya zetu mara kwa mara
kwa baadhi ya magonjwa haya hususani shinikizo la damu halina dalili za moja
kwa moja lakini kama utafanya upimaji itasaidia kubaini changamoto na kuanza
matibabu mapema,” amesema Prof. Janabi.
Kwa upande wake Mratibu wa mafunzo hayo, Prof. Pilly Chillo
amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wataalam mbalimbali namna ya
kufanya vipimo na kuwabaini wagonjwa wenye changamoto za magonjwa ya moyo hivyo
kurahisha huduma katika maeneo yao ya kutolea huduma.
Mafunzo hayo ya wiki nne yamehusisha washiriki kutoka
Somalia, Gambia, Eswatini, Zanzibar na wenyeji Tanzania ambapo yameshirikisha
washiriki 45 wa mataifa husika.
0 Maoni