Moto wateketeza mali na kutia hasara wafanyabiashara Kariakoo

 

Moto umeunguza majengo kadhaa, maduka, vibanda na migahawa katika eneo la Kariakoo Jijini Dar es Salaam, na kuwaacha wafanyabiashara wakiangua vilio, hali iliyobua taharuki kwa muda katika eneo hilo ambalo ni kitovu cha biashara.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila alifika katika eneo hilo la moto na kuwaeleza waandishi wa habari kwamba moto huo ulianza katika jengo moja na baadae majengo machache yakashika moto.

Amesema kuwa hadi majira ya saa nne asubuhi hakukuwa na taarifa yoyote ya mtu aliyepoteza maisha katika tukio hilo la moto, lakini kuna baadhi ya watu watapata hasara za mali na majengo yaliyoungua moto.

Ameongeza kuwa wamebaini kati ya jengo na jengo vichochoro vimezibwa, na uongozi ulishaagiza vichochoro hivyo vizibuliwe ili kuwezesha kupatikana namna ya kupita pindi panapotokea janga la moto ili kuwe na namna ya kuzima.

"Nyinyi wenyewe (waandishi wa habari) mmeona vichochoro vimezibwa na mabanda, na mabanda yenyewe yamejengwa kwa mbao jambo ambalo limesaidia kuchochea kuwaka zaidi kwa moto uliotokea," alisema RC Chalamila.

Chalamila amevipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kulinda mali na raia, pamoja na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, “Wamejitahidi sana, mpaka muda huu zimamoto wamekata moto usiendelee kwenye majengo mengine na kuendelea kuzima majengo yaliyoungua.”

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo moto huo ulianza majira ya saa 12 alfajiri, ambapo majirani walihaha kuwapigia simu wahusika ili kuwahi kuokoa bidhaa zao ambapo baadhi yao walifanikiwa kuokoa bidhaa na wengine walishindwa baada ya moto kushika kasi.

Jeshi la Polisi lilionekana likiwa limeimarisha ulinzo katika eneo hilo lililotokea moto ili kudhibiti wahalifu wasifanye vitendo vya kupora bidhaa katika maduka hayo, wakisaidiana na wananchi waliokuwapo.

Kufuatia moto huo barabara ya Mtaa wa Msimbazi ilifungwa kwa muda kwa zaidi ya saa tatu baada ya kutokea moto huo, ambapo watumiaji wa barabara hiyo walilazimika kutumia barabara mbadala kwa muda.



Chapisha Maoni

0 Maoni