WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Watanzania
walioshiriki katika Jukwaa la Tatu la Biashara na Uwekezaji baina ya Tanzania
na Italia wahakikishe wanatumia vizuri fursa walizozipata kutoka kwenye jukwaa
hilo, ikiwa ni pamoja na kutoa ushirikiano kwa wawekezaji na wafanyabiashara
walioonesha nia ya kuja kuwekeza nchini.
Pia, Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita
inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeondoa tozo na
urasimu uliokuwepo awali kwa lengo la kurahisisha shughuli za biashara na
uwekezaji nchini.
Kadhalika, Waziri Mkuu ametoa wito kwa Watanzania wanaoishi
nje ya nchi wahakikishe Taifa linanufaika kwa kuwa mabalozi wazuri wa kutangaza
vivutio vya uwekezaji pamoja na kuwashawishi wawekezaji kutoka katika nchi
wanazoishi waje kuwekeza Tanzania.
Ameyasema hayo jana katika hafla ya chakula cha mchana
iliyoandaliwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Italia kwa kushirikiana na Benki ya
NMB kwa lengo la kuwatambua wafadhili na washiriki wa Jukwaa la Tatu la
Biashara na Uwekezaji baina ya Tanzania na Italia.
Waziri Mkuu ambaye yuko Italia akimuwakilisha Mheshimiwa
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Jukwaa la Kimataifa la Chakula
Duniani ulioanza Oktoba 16 hadi Oktoba 20, 2023, Rome nchini Italia,
aliwasisitiza Watanzania waheshimu sheria za nchi husika.
Mheshimiwa Majaliwa alisema kupitia jukwaa hilo
wafanyabiashara na wawekezaji wengi kutoka nchini Italia wameonesha nia ya kuja
Tanzania kwa ajili ya kuwekeza katika sekta mbalimbali ikiwemo ya kilimo, hivyo
amewataka viongozi na watendaji wa wizara zinazohusika na masuala ya uwekezaji
kuchangamkia fursa hiyo.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu ametoa wito kwa wafugaji nchini
wakubali kubadilika na wafuge kwa kutumia teknolijia ya kisasa ili waweze
kujinufaisha zaidi na shughuli hiyo. “Tubadilike tupate manufaa zaidi, ufugaji
ni uchumi, ufugaji ni maisha na ufugaji ni kazi, hivyo tubadili mfumo wa
ufugaji wetu kwa ajili ya kujiongezea kipato zaidi.”
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo ya
Biashara Tanzania (TanTrade), Latifa alisema mamlaka yao imefaidika sana kwa
kushiriki katika jukwaa hilo kwa sababu sekta zote walizozitangaza zikiwemo za
ujenzi, viwanda zimeonesha kufurahiwa na wadau wa uwekezaji, hivyo wamejipanga
kupokea wafanyabiashara.
Awali, Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mheshimiwa Balozi
Mahmoud Thabit Kombo amemshukuru Mheshimiwa Majaliwa kwa kushiriki katika
jukwaa hilo na kwamba ofisi hizo za Ubalozi wa Tanzania nchini Italia zitatoa
ushirikiano kwa wafanyabiashara na wawekezaji wote waliokuwa tayari kuja
kuwekeza na kufanya biashara nchini.
CHANZO: Ofisi ya Waziri Mkuu
0 Maoni