Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetoa maagizo matatu kwa
Serikali kupitia Wizara ya Kilimo na taasisi zilizoko chini yake, hususan,
Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea
Tanzania (TRFA) yakilenga kuweka mazingira mazuri kwa wakulima nchini kuzalisha
zaidi, wanapojiandaa kuanza msimu mwingine wa kilimo, mwaka huu.
Maagizo hayo ya CCM yaliyotolewa na Katibu Mkuu wa Chama
hicho, Komredi Daniel Godfrey Chongolo, ni pamoja na Wizara ya Kilimo kuweka na
kutangaza utaratibu wa kulipa malipo ya wakulima wa mahindi, hususan wa mikoa
ya Kusini, ukiwemo Mkoa wa Rukwa, ambao mazao yao yalinunuliwa na NFRA na
hawajamaliza kulipwa.
Agizo jingine ni kuitaka Wizara ya Kilimo kupitia NFRA kutoa
fedha za kununua mahindi ya wakulima ambayo bado yako kwenye maghala huku msimu
mwingine wa kilimo ukikaribia kuanza, hali inayoweza kuathiri uzalishaji wao.
Ndugu Chongolo pia ameagiza Wizara ya Kilimo, kupitia TRFA
kuhakikisha wakulima wanapata mbolea ya ruzuku mapema kabla ya msimu kuanza na
waipate katika maeneo ya karibu, tofauti na msimu uliopita ambapo kulikuwa na
malalamiko ya wananchi kuwa mbolea hiyo ilichelewa kufika na walilazimika
kuifuata umbali mrefu kuipata.
“Kuna suala la malipo ya mahindi…tunaiagiza Wizara ya Kilimo
kuwalipa wakulima wa mahindi yaliyonunuliwa na NFRA haraka ili waweze kujiandaa
na msimu wa kilimo unaokuja. Lakini pia tunawaagiza Wizara ya Kilimo walete
fedha ili NFRA wanunue mahindi ambayo bado yako kwa wakulima”.
“Mmemsikia mara kadhaa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan
akisisitiza suala la kuhifadhi chakula. Kwa mujibu wa wataalam wetu wa utabiri
wa hali ya hewa, kuna dalili za kuwepo kwa El Nino kwenye msimu huu wa mvua,
ambayo inaweza kuathiri uzalishaji. Hivyo Serikali lazima iweke mpango wa
kununua chakula cha kutosha ili kuwa na uhakika wa chakula,” amesema Chongolo
na kuongeza;
“Agizo jingine ni kuhusu mbolea…tunawaagiza wasogeze mbolea
karibu ili ipatikane kwa karibu kwa wananchi. Huko nyuma, sehemu kubwa ilishia
kupatikana makao makuu ya wilaya. Tunawataka Wizara ya Kilimo wafanyie kazi
haya.”
Ndugu Chongolo ametoa maagizo hayo leo Jumatano, Oktoba 11,
2023, alipokuwa akihutubia mkutano mkubwa wa hadhara katika Uwanja wa Mandela,
Sumbawanga mjini, mkoani Rukwa, alipokuwa akihitimisha ziara yake ya siku 4 katika
mkoa huo.
Maagizo hayo ya Katibu Mkuu Chongolo, yamekuja siku chache
baada ya Kiongozi huyo kukutana na malalamiko ya wakulima wa mahindi mara tu
alipoanza ziara yake Mkoa wa Rukwa, wilayani Nkasi, Oktoba 8, mwaka huu, akiwa
ametokea katika Mkoa wa Katavi, akiendelea na ziara zake za kukataa miradi ya
maendeleo, ambayo ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020 - 2025,
kuhamasisha uhai wa CCM katika ngazi ya mashina na kusikiliza changamoto za
wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.
Mbali na maagizo hayo, Katibu Mkuu Chongolo pia alizungumzia
umuhimu wa viongozi na watendaji wa Chama na Serikali katika ngazi mbalimbali,
kushuka kwenda kwa wananchi kuwasikiliza changamoto zao na kuzitafutia
majawabu.
Chongolo amewataka viongozi wa serikali kuhakikisha
wanawahudumia wananchi na kutatua changamoto zao ili kuendelea kutekeleza nia
na dhamira njema ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu
Hassan ya kuwatumikia Watanzania na kuyafikia malengo yanayokusudiwa.
Chongolo amesema katika maeneo waliotembelea kuna miradi
ambayo imekamilika lakini kuna maeneo ambayo miradi haijakamilika hivyo wametoa
maelekezo kwa viongozi husika kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa haraka,
kadri ilivyopangwa.
Amesema miradi hiyo ni pamoja na ile inayohusu huduma ya
maji ambapo wametoa maelekezo mahsusi kuhakikisha inakamilika na wananchi
wanapata maji.
Kwenye eneo la elimu amesema kazi kubwa imefanyika na
inaendelea kufanyika, ambapo mabilioni yaliyoshushwa kwa kipindi hiki kifupi
shule zimejengwa kwenye kila kata na watoto wanaendelea kupata elimu bila
malipo.
Kwa upande wa nishati ya umeme mkoani Rukwa, Ndugu Chongolo
amesema hapo kabla ulikuwa na changamoto lakini kwa sasa imepungua kwa kiwango
kikubwa kutokana na serikali kuwekeza kwenye mpango wa kusambaza umeme
vijijini, ambapo vijiji vilivyobaki ni chini ya 30 hivyo ameelekeza mpaka
kufika Disemba 30 vijiji vyote 339 mkoani humo, vipate umeme.
Amesema maelekezo ya Rais ni kuhakikisha umeme unamfikia
kila mwananchi, ndiyo maana Mhe. Samia Suluhu Hassan ameagiza kuongezwa Kwan
hizo za umeme kutoka 20 kila kijiji hadi 60 ili kuongeza wigo wa upatikanaji
wake kwa kila kijiji kilichofikiwa, hatimae Keri ya ukosefu wa nishati hiyo,
Uwe historia.
“Kazi mnafanya, kikubwa ni wajibu wa serikali kuleta miradi
ili mneemeke na shughuli mnazofanya, kuna suala la mahindi wapo watu
wawajalipwa tunaiagiza wizara ya kilimo kuwalipa haraka ili watu waendelee na
msimu ujao wa kilimo.”
“Tunaiagiza tena Wizara ya kilimo wahakikishe mahindi
yailiyoko kwa wananchi yananunuliwa na mbolea mwaka huu waisogeze kwa wananchi
sio iishie wilayani.”
Aidha, Chongolo ametoa kwa Naibu Waziri TAMISEMI kuhakikisha
wanajenga vituo vya afya Senga na Sumbawanga Asili ili kutatua changamoto ya
wananchi kukosa vituo vya afya katika maeneo hayo.
Pia amewataka Viongozi wa Chama cha Mapinduzi katika mkoa
huo wajenge mazingira ya wananchi kuwafikia na kueleza changamoto zao.
0 Maoni