Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sana na Michezo Bw. Gerson
Msigwa ameikabidhi timu ya Twiga Stars kitita cha Sh. Milioni 10 zilizotolewa
na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan
kufuatia ushindi waliopata dhidi ya timu ya Ivory Coast uliowawezesha kufuzu
michuano ya WAFCON 2024.
Akikabidhi fedha hizo, Katibu Mkuu Bw. Msigwa amesema
wachezaji hao wanafanya kazi kubwa ya kuiwakilisha nchi Kimataifa na Serikali
ipo pamoja nao kwa kuwa wanaitangaza na kuipigania nchi yao.
“Mnapokuwa uwanjani katika mechi za kimataifa mnakuwa
mmebeba matumaini ya watanzania, katika mechi zote mlizocheza tumeona dhamira
mliyonayo kwa nchi yenu, Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anawapongeza sana,
anafurahi sana anapowaona mnacheza uwanjani, anafurahi sana mnapopata matokeo
mazuri katika mechi zetu” Katibu Mkuu Bw. Msigwa.
Kwa upande wake Kocha Mkuu wa timu hiyo Bakari Shime amesema
amefurahi kupokea kwa kiasi hicho cha fedha kutoka kwa Mama Samia kuhamasisha
vijana hao kujituma zaidi kupambania nchi yao lakini kubwa kwa vijana hao ni
pale kuona Rais anatambua mchango wao.
“Fedha ni sehemu kubwa ya hamasa, kitendo cha Rais Samia
kuwafuatilia vijana wetu na kutambua timu hiyo inacheza ni faraja kubwa kwao na
imekuwa chachu ya kujituma wakiamini kuwa Mama yupo pamoja nao,” amesema Shime.
Nahodha wa Twiga Stars, Joyce Lema amesema wanamshukuru Rais
Samia kwa kuzidi kuwapa hamasa na kumuahidi kutomuangusha katika mashindano
yote yaliyopo mbele yao.
“Kwa hamasa hii inaonyesha kuwa kuna kitu kimeongeza katika
soka na wanawake, tunatamani siku moja viongozi kuendelea kujitokeza kwa wingi
kusapoti soka la wanawake kama ilivyo kwa wanaume,” amesema Joyce.
0 Maoni