Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeishauri
Serikali kuweka kipaumbele katika kusambaza Vituo vya Nishati ya Gesi
Iliyoshindiliwa (CNG) inayotumika katika kuendesha mitambo na magari nchini ili
kukabiliana na gharama za mafuta pale zinapotokea.
Ushauri huo umetolewa jana Jijini Dodoma na Mwenyekiti wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Mhe. Mathayo David wakati Kamati
hiyo ilipopokea taarifa ya Wizara ya Nishati, kuhusu hatua iliyofikiwa katika
utekelezaji wa mradi wa kuanzisha vituo hivyo.
“Tunashauri Serikali iweke kipaumbele katika matumizi ya
gesi asilia katika maeneo mbalimbali nchini pamoja na matumizi mengine ili
Watanzania waweze kupata huduma hiyo kwa urahisi,” amesema Mwenyekiti wa Kamati
Mathayo David.
Katika hatua nyingine, Mhe. Mathayo ameipongeza Serikali kwa
mikakati mizuri ya uanzishwaji wa karakana za kubadili mifumo ya matumizi
kutoka kwenye mafuta na kwenda kwenye gesi asilia kwenye magari hali inayochochea
matumizi ya gesi asilia nchini kwa wingi.
"Uwepo wa karakana hizi kwa wingi utarahisisha utoaji
wa huduma za ubadilishaji mifumo na ukarabati wa hitilafu kwa muda mfupi na
karakana hizi zitumie teknolojia ya kisasa wakati wa kubadili magari na
mitambo,” ameeleza Mhe. Mathayo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,
Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema Serikali imepokea ushauri wote uliotolewa na
kamati ili kuweza kuboresha Sekta ya Nishati nchini.
Amesema, Wizara imedhamiria kuchochea matumizi ya Gesi
Asilia iliyoshindiliwa kwa maeneo pia yaliyo mbali na mtandao wa mabomba pamoja
na matumizi ya gesi hiyo kwenye magari kwa kuwa na vituo vingi vya kujazia gesi
kwenye magari.
Viongozi mbalimbali walioshiriki katika kikao hicho ni
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mha. Felchesmi Mramba, Naibu Katibu Mkuu Wizara
ya Nishati, Bw. Athumani Mbuttuka, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu Mha.
Innocent Luoga na Watendaji kutoka Wizara na Taasisi.
0 Maoni