Naibu Waziri wa Nishati, Mhe.Judith Kapinga amesema kuwa, shilingi Bilioni 163 zitatumika kuunganisha Mkoa wa Katavi katika Gridi ya Taifa na hivyo kuwezesha mkoa huo kupata umeme wa uhakika na unaotabirika.
Mhe. Kapinga amesema hayo wakati akizungumza na Wananchi wa
Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi wakati wa ziara Katibu Mkuu wa Chama cha
Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo mkoani humo tarehe 7 Oktoba 2023.
Kapinga amesema kuwa, mradi huo unatarajiwa kukamilika mwezi
Juni mwaka 2024 na kutoa onyo kuwa, watakaosababisha mradi huo kutokukamilika
kwa wakati uliopangwa watachukuliwa hatua.
"Wizara ya Nishati haitakuwa na kikwazo kuhakikisha
Katavi inapata umeme mwingi na wa uhakika kwa kuwa tayari tumejipanga na fedha
zipo, yeyote akayeshindwa kutekeleza mradi huo kwa wakati, ufanisi na weledi
kama ilivyoelekezwa atachukuliwa hatua kali za kisheria,"alisema Mhe.
Kapinga.
Ameeleza kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha hizo ili kuhakikisha kuwa Mkoa wa Katavi
unapata umeme wa uhakika na kuondokana na umeme unaozalishwa kwa kutumia mafuta
kwani una gharama kubwa.
Amesema fedha hizo zitatumika katika kujenga mradi wa njia
ya kusafirisha umeme kutoka mkoani Tabora hadi Katavi pamoja na vituo vitatu
kupoza na kusambaza umeme vya Ipole, Inyonga na Uhuru ambapo Kituo cha Uhuru kilichopo
wilayani Urambo mkoani Tabora ujenzi wake unaendelea vizuri na umefikia
asilimia 60 ya utekelezaji wake.
Kuhusu njia ya kusafirisha umeme amesema ujenzi wake
umefikia 40%, na kwamba vifaa vyote vinavyohitajika katika eneo la mradi
vitakuwa vimefika katika maeneo ya kazi ifikapo mwishoni mwa mwezi Oktoba, ili
mwezi Juni 2024, umeme wa gridi uwe umefika Katavi.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri amekagua ujenzi wa Kituo
cha Kupoza na Kusambaza umeme cha Mpanda kinachojengwa na Kampuni ya Tanzu ya
Shirika la Umeme Tanzania ya ETDCO inayohusika na ujenzi wa miundombinu ya
usafirishaji ya umeme na kuwataka waongeze kasi ya ujenzi wa njia ya
kusafirisha umeme wanayoitekeleza.
Ameiagiza kampuni hiyo kuwa, ikifikapo Mwezi wa 10 mwishoni
nguzo zote za zege ambazo zinahitajika ziwe zimefika katika maeneo ya kazi
(site) na kusimikwa na kwamba atafuatilia utekelezaji wake na kwa sababu
kampuni hiyo imepewa fedha shilingi Bilioni 58 ili kuwaongezea ufanisi.
“Kwa ujumla tumekubaliana vifaa vya kazi vyote
vinavyohitatija katika kazi hii, ikifika mwezi wa 12 viwe vimefika, na tutafika
kuvikagua, pia tutakagua kazi inayotekelezwa na kazi kama haijafanyika kama
tulivyokubaliana tutachukuwa hatua; kwa sababu kampuni hii ni ya ndani
inatakiwa kufanya kazi kwa mfano mzuri ili iweze kuchagiza kampuni nyingine
kufanya kazi kwa weledi na kwa ufanisi mkubwa sana, iwe jua iwe mvua ni lazima
tukubaliane na tutekeleze yale tuliokubaliana bila kisingizo chochote, ikifika
Mwezi Juni 2024 mradi huu uwe umekamilika na Katavi kuunganishwa katika
Gridi ya Taifa," amesisitiza Mhe. Kapinga.
Na. Zuena Msuya na MayLoyce Mpombo- Katavi
0 Maoni