WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Kamanda wa TAKUKURU
mkoa wa Kigoma, Steven Mafiga afanye haraka kuwachunguza Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza, Bi. Zainab Mbunda na Mweka Hazina wa Wilaya
hiyo, Bw. Majjid Mabanga ili kubaini ni kwa nini miradi haiendi wakati fedha
zilishatolewa kitambo.
"Kamanda wa TAKUKURU Mkoa kamilisha hiyo kazi kwa
haraka sana. Rais wetu analeta fedha nyingi sana lakini kuna watu hawafanyi
maamuzi. Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri na Mweka Hazina wakae pembeni
kupisha uchunguzi, wakati ukiendelea na kazi," amesema.
Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo jana mchana wakati
akizungumza na watumishi na wananchi waliohudhuria uwekaji wa jiwe la msingi
kwenye jengo la ghorofa moja la Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza, lililoko
Lugufu, Uvinza, mkoani Kigoma.
Waziri Mkuu amechukua hatua hiyo baada ya kubaini kuwa fedha
za miradi ya ujenzi wa hospitali ya wilaya, vituo vya afya vya Rukoma na Sunuka
na zahanati za Mgambo na Kajeje zilizotumwa tangu mwaka 2021/2022, zinadaiwa
kuwepo kwenye akaunti wakati majengo husika hayajakamilika na taarifa
inayotolewa inasema ujenzi uko kwenye hatua ya ukamilishaji.
"Kwa nini lugha ya ukamilishaji hapa Uvinza imeshamiri?
Fedha za miradi zikiletwa ziende kwenye kazi iliyokusudiwa. Sasa hapa,
Mkurugenzi anasema fedha zipo, Mweka Hazina anasema zimeisha, Mhandisi
aliandika dokezo la kuomba vifaa, mtu wa manunuzi anasema hajalipata. Fedha
zipo na kazi haziendi. Nimewaweka pembeni kwa sababu nimeona usimamizi ni
mbovu," amesema.
"Leo hii tukitoka Nguruka, Kamanda wa TAKUKURU ingia
kazini, angalia hizo fedha ziko kwenye akaunti zipi, angalia kuna shilingi
ngapi na zilikuwa zimepangwa kufanya shughuli gani."
Kabla ya kuweka jiwe la msingi la jengo la ofisi ya
Halmashauri hiyo, Waziri Mkuu alikagua hospitali ya wilaya hiyo na kubaini
majengo kadhaa hayajakamilika licha ya kuwa fedha zilitolewa tangu Mei, 2021.
Pia alikuta vifaa tiba vingi vikiwa kwenye chumba ambacho hakina milango wala
vipoza hewa (Air conditioner) huku vikiwa vimejaa vumbi. “Ni kwa nini vifaa
hivi kwa kielektroniki tena vya gharama kubwa vimeachwa tu hapa, tena vinapigwa
na vumbi? Hamuoni huruma kwa fedha za Serikali?” alihoji.
Waziri Mkuu amesema ametembelea mikoa mbalimbali hapa nchini
na kuweka mawe ya msingi ama kuzindua majengo ya wagonjwa wa dharura (EMD)
lakini haelewi ni kwa nini majengo ya Uvinza hadi leo hayajakamilika. “Kibondo
na Kasulu wenzenu wamekamilisha majengo yao, iweje hapa Uvinza bado tu?”
alihoji Waziri Mkuu.
Akitoa taarifa kuhusu ujenzi wa hospitali ya wilaya, Mkuu wa
Kituo kwenye hospitali hiyo, Dkt. David Patrick alisema mwaka 2019 walipokea
sh. bilioni 1.5 za ujenzi wa majengo saba, kisha wakapokea sh. milioni 300 za
njia ya watembea kwa miguu. “Mei, 2021 tulipokea shilingi milioni 500 za wodi
tatu, na Machi, 2022 tulipokea shilingi milioni 390 za EMD na nyumba ya
watumishi. Pia tulipokea shilingi milioni 523 za vifaa tiba,” alisema.
“Halmashauri ya Wilaya Uvinza ilipokea fedha kiasi cha sh.
bilioni moja na milioni mia tano mwaka 2019 kwa ajili ya ujenzi wa majengo saba
ya awali ambayo ni jengo la mionzi, wodi ya wazazi, maabara, wagonjwa wa nje,
utawala, madawa, jengo la kufulia. Utekelezaji wa mradi wa Hospitali ya Wilaya
ulianza tarehe 10 Januari, 2019,” alisema Dkt. Patrick..
Mapema, Naibu Waziri wa TAMISEMI (Afya), Dkt. Festo Dugange
alisema Serikali ilitoa sh. bilioni 1.9, kisha ikatoa sh. milioni 170 na Julai,
mwaka huu imetoa milioni 750 kwa ajili ya ujenzi jengo la Halmashauri ambalo
hadi sasa lilipaswa kuwa limekamilika. “Nawapa muda hadi tarehe 30 Oktoba, 2023
liwe limekamilika na limeanza kutoa huduma,” alisema.
Kuhusu hospitali ya wilaya ya Uvinza, Dkt. Dugange alisema
fedha zilianza kutumwa mwaka wa fedha 2019/2020 na hadi sasa sh. bilioni 3.4
zimeshapokelewa. “Julai 2021 tulikuja kukagua na kuelezwa kuwa majengo
yangekamilika ifikapo Desemba, 2021. Shilingi milioni 300 za EMD zilitumwa
lakini bado jengo hilo halikamilika."
0 Maoni