WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa leo Septemba 20, 2023 amefungua
Kongamano la Tano na Maonesho ya Nishati Tanzania na amesema kwamba Serikali
imedhamiria kuwa mzalishaji mkubwa na nishati.
“Tunaendelea na utafutaji wa gesi, tunataka tuwe wazalishaji
wakubwa wa nishati, tuwe na umeme wa kutosha utakaopatikana kwa urahisi na
nafuu na ziada tutauza nje ya nchi,” alisema Majaliwa.
Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo baada ya kufungua
kongamano hilo la siku mbili linalofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha
Mikutano cha Julius Nyerere, Dar es Salaam.
Amesema kuwa Tanzania haitegemei kuzalisha umeme kwa kutumia
maji pekee bali inaendelea kuweka mkazo katika uzalishaji wa umeme kwa kutumia
nishati nyingine kama gesi na jua.
Waziri Mkuu amesema katika kongamano hilo la kimataifa la
nishati ambalo limehusisha viongozi na wadau kutoka katika mataifa mbalimbali
Duniani litajadili namna bora ya kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa
nishati.
Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa kuzisisitiza nchi zote
wanachama kuhakikisha taasisi za mafunzo zinatoa programu maalum za mafunzo
katika sekta za nishati ili kuongeza idadi ya watu walio na ujuzi na maarifa
kwenye sekta hiyo.
Amesema kuwa nishati ni sekta muhimu katika kufikia lengo la
uanzishwaji wa viwanda na katika kuimarisha na kuwezesha uzalishaji na shughuli
nyingine za kiuchumi. “Lazima tufanye kazi kwa ushirikiano na wadau wote ili
kufungua fursa kwa Watanzania wote.”
Amesema ili kuwaendeleza wafanyabiaahara wa ndani na Watanzania
kushiriki katika sekta ya nishati, Serikali itaendelea kuhakikisha kanuni na
taratibu zinazofaa zinawekwa ili kuwezesha ushirikishwaji katika mnyororo wa
thamani wa maendeleo kwenye sekta ya nishati
Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,
Dkt. Doto Biteko amesema wameendelea kutekeleza mipango mbalimbali waliojiwekea
katika kuhakikisha umeme unapatikana wakati wote nchini.
Dkt. Biteko amesema zaidi ya kampuni 100 za nishati kutoka
katika maeneo mbalimbali duniani zinashiriki katika kongamano hilo ambalo
lilitanguliwa na mkutano wa viongozi wa nishati.
0 Maoni