Bodi ya wadhamini TANAPA iliyozinduliwa takribani wiki
chache zilizopita ikiongozwa na Mwenyekiti wake Jenerali Mstaafu George Waitara
wametembelea Hifadhi ya Taifa Arusha na kufahamishwa kuwa hifadhi hiyo iko
mbioni kuanzisha zao jipya la utalii lijulikanalo kama "Canyoning"
ili kuongeza idadi ya watalii na kufikia adhma ya serikali ya watalii milioni
5. Ziara hiyo imefanyika jana hifadhi hiyo iliyopo jijini Arusha.
Zao hili jipya la utalii litakuwa ni la kwanza Tanzania na
Afrika Mashariki kuanzishwa katika Hifadhi za Taifa na Mapori ya Akiba,
linatarajiwa kuvutia watalii wengi zaidi kutembelea hifadhi hiyo. Baadhi ya
nchi duniani zenye utalii wa "Canyoning" ni Afrika ya Kusini na nchi
ya Croatia inayopatikana katika bara la Asia.
Aidha, Mwenyekiti huyo wa Bodi ya Wadhamini TANAPA
ameipongeza Menejimenti ya Hifadhi ya Taifa Arusha kwa kubuni mazao mapya ya
utalii kama vile Geopark na ujio huu mpya wa "canyoning", mazao haya
yataongeza idadi ya watalii na mapato kwa TANAPA na taifa kwa ujumla.
Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Yustina Kiwango, Mkuu wa
Hifadhi ya Taifa Arusha alielezea lengo la uanzishwaji wa "Canyoning"
ni mkakati wa TANAPA kubuni mazao mapya na kuongeza mapato kwa shirika na
Taifa. Hata hivyo alieleza kuwa "Canyoning" ni utalii wa kutembea
katika mito yenye kina kifupi na mabonde, maporomoko ya maji na kuruka katika
miamba iliyo chini ya kivuli cha uoto wa asili.
Hifadhi ya Taifa Arusha ni miongoni mwa hifadhi 21
zinazosimamiwa na TANAPA ikisheheni maziwa yaliyo na utajiri wa ndege aina
Flamingo pamoja na Kreta ya Ngurudoto iliyojaa Wanyamapori kama twiga, tembo,
nyati, Mbega na aina tofauti ya ndege wakaazi na wahamao.
Na. Philipo Hassan - Arusha
0 Maoni