Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu
Hassan, amesema Dk. Salim Ahmed Salim ni Mtanzania mahiri na mashuhuri
aliyetoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Tanzania na bara zima la Afrika.
Rais Samia ameyasema hayo leo katika hafla ya kuzindua
Tovuti ya Hifadhi ya Nyaraka za Kumbukumbu za Kidigitali za Dk. Salim Ahmed
Salim, iliyofanyika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC)
jijini Dar es Salaam.
Amesema kwamba katika nyanja ya Kidiplomasia Dk. Salim aliliwakilisha
vyema taifa la Tanzania, katika nchi mbalimbali zikiwamo Misri, India, China,
Marekani, katika Umoja wa Mataifa na Umoja wa Nchi Huru za Afrika (AU) na
kwingineko.
“Dk. Salim alijitahidi sana kuhuisha mahusiano mazuri baina
ya Tanzania na nchi nyingine pamoja na taasisi alizohudumu, akiwa balozi wa Tanzania
nchini India alihamasisha serikali ya India ya Waziri Mkuu wa wakati huo Indra
Gandhi kuanzisha viwanda vidogo vidogo nchini,” alisema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia amesema uwakilishi mahiri wa Dk. Salim nchini
China uliimarisha sana mahusiano baina ya nchi hizi na kupelekea Baba wa Taifa Hayati
Julius Kambarage Nyerere kuwa rais wa kwanza kutoka Afrika kufanya ziara nchini
China.
“Mahusiano mazuri haya baina ya China na Tanzania yalisaidia
kufanikisha uanzishwaji wa viwanda mbalimbali kikiwamo kiwanda cha nguo cha
Urafiki (Urafiki Textile Industries) na baadae ujenzi wa reli ya TAZARA nchini,”
alisema Rais Samia.
Amesema wakati Dk. Salim alipokuwa mwakilishi wa Tanzania
kwenye Umoja wa Mataifa alichangia kwa kiasi kikubwa katika harakati za
ukombozi na mpango wa kuirudishia China kiti chake cha kudumu kwenye Baraza la
Usalama la Umoja wa Mataifa.
“Mpango wa kuirudishia China kiti cha kudumu kwenye baraza
la Usalama la Umoja wa Mataifa ulimugharimu Dk. Salim pamoja na sababu zingine za
kukosa kwake nafasi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,” alisema Rais Samia na kuongeza,
“Pamoja na sababu zingine za kuambiwa kuwa mweusi hawezi kushika nafasi hiyo,
lakini kulikuwa na sababu zingine moja wapo likiwa hili la Dk. Salim kusimama
kidete na nchi ya China.”
Amesema kwa upande wa nchini, Dk. Salim amelitumikia taifa
katika nafasi mbalimbali kama vile Waziri Mkuu, Waziri wa Mambo ya Nchi, Waziri
wa Ulinzi na nafasi zingine alizopewa na alichapa kazi kwa moyo wake wote na
kudhihirisha uongozi wake uliojaa uadilifu.
Katika hafla hiyo Rais Samia ametangaza kubadilisha jina la
Chuo cha Diplomasia nchini na kukipa jina la Waziri Mkuu Mstaafu Dk. Salim
Ahemd Salim, ambapo sasa Chuo hicho kitakuwa kinaitwa Dr. Salim Ahmed Salim
Centre for Foreigh Relations.
0 Maoni