Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) Gianni Infantino
amesema kuwa anaielewa vizuri Tanzania na kuahidi kuwa atakuwapo kwenye
uzinduzi wa michuano ya Africa Super League itakayofanyika nchini, Jijini Dar
es Salaam.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya
Klabu ya Simba, Salim Tryagain, ambaye amekutana na Infantino pamoja na
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu FIFA Omella Desiree Bella.
Tryagain ameeleza hayo kupitia kwenye ukurasa wa akaunti
yake ya mtandao wa twitter na kuongeza kuwa amejadiliana na viongozi hao wa
FIFA kuhusu michuano ya Africa Super Legue, akiwa huko Park Hyatt, Jijini
Sydney nchini Australia.
Tryagain yupo Sydney kushiriki kozi ya Diploma katika
uongozi na klabu inayotolewa na FIFA (Diploma in Club Management), pia
kujifunza shughuli za mpira na jinsi mashindano makubwa yanavyoandaliwa.
Timu ya Simba ndio timu pekee ya Tanzania itakayoshiriki
mashindano hayo, timu nyingine ni Petro de Luanda- Angola, TP Mazembe- DR Congo,
Al Ahly- Egypt, Horoya- Guinea, Wydad Casablanca- Morocco, Esperance- Tunisia
na Mamelodi Sundowns- Afrika Kusini.
0 Maoni