Rais Dk. Mwinyi alipongeza Kanisa la Anglikana kwa kuendeleza amani nchini

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi amelipongeza Kanisa la Anglikana Tanzania kwa kuendeleza amani, umoja na mshikamano nchini.

Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo alipokutana na Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Maimbo Mndolwa na ujumbe wake waliofika Ikulu Zanzibar kujitambulisha baada ya kuchaguliwa mwezi Februari mwaka huu kuliongoza Kanisa hilo kwa kipindi cha miaka mitano.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi amewashukuru viongozi wa kanisa hilo kwa mipango yao ya kuitangaza Zanzibar katika sekta ya utalii na Serikali ipo tayari kuendeleza ushirikiano na kanisa katika sekta hiyo.

Naye Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania Maimbo Mndolwa amempongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar.

Vilevile Askofu Mndolwa amesema kanisa linaendelea kumuombea katika uongozi wake.

🗓️30 Agosti, 2023

📍Ikulu, Zanzibar.

Chapisha Maoni

0 Maoni