Kamati ya Bunge ya Ustawi wa Maendeleo ya Jamii imempongeza
Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha ustawi wa vijana na Watu wenye
Ulemavu kujikwamua kiuchumi.
Kauli hiyo imetolewa jana bungeni na
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Fatuma Toufiq kwenye kikao cha kamati cha
kupokea taarifa ya utekelezaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana pamoja na
utekelezaji wa Programu ya Taifa ya Ukuzaji Ujuzi inayoratibiwa na Ofisi ya
Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.
Aidha, Mhe. Fatuma Toufiq amesema kamati hiyo itaendelea
kuishauri Serikali kuendelea kuongeza wigo wa kuwezesha vijana wengi zaidi
kupata mikopo, fursa mbalimbali zinazotolewa na serikali.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu –
Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Prof. Joyce Ndalichako ameeleza kuwa Ofisi
yake imefanya maboresho ya mwongozo wa mfuko huo mwaka 2023 ili kupanua wigo wa
viwango vya mkopo inayotolewa sambamba na kumwezesha mtu moja moja kukopa
badala ya kikundi.
Naye, Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Prof. Jamal Katundu amesema
kuwa, ofisi hiyo imetenga Sh. Bilioni moja katika mfuko wa Watu wenye Ulemavu
kwa ajili ya utekelezaji wa afua mbalimbali za kundi hilo.
0 Maoni