Hii kali wahamiaji haramu 65 wasafirishwa kwenye tanki la mafuta!

 

Tatizo la usafirishaji wahamiaji haramu kwa mbinu mbalimbali limezidi kuchukua sura mpya, baada ya kukamatwa kwa wahamiaji 65 kutoka nchi ya Ethiopia wakiwa ndani ya tanki la lori la mafuta.

Wahamiaji hao haramu walikamatwa jana na Idara ya Uhamiaji, wakati wakisafirishwa kutokea mkoa wa Mwanza kuelekea Tunduma hadi walipokamatwa mkoani Katavi.

Hata hivyo kama ilivyo kwa matukio mengine, haijajulikana wahamiaji hao waliwezaje kuingia nchini hadi Mwanza bila kujulikana mpaka walipokamatwa.

Kwa muda sasa Tanzania imekuwa ikiwakamata wahamiaji haramu, wengi wao wakitokea nchini za Ethiopia na Eritrea wakiwa washaingia kati kati ya nchi, kwa kutumia njia za panya mipakani.

Hata hivyo mbinu za awali za usafirishaji zilihusisha wahamiaji kuwekwa kwenye makasha (kontena) ama kwenye malori ya mizigo lakini safari hii limetumika tanki la lori la mafuta.

Hii inaonesha kwamba, wahalifu wanaofanya biashara ya usafirishaji wahamiaji haramu wamekuwa wakibuni mbinu mpya kila siku ili kuvikwepa vyombo vya dola.

Wahamiaji hao waliokamatwa majira ya mchana katika kizuizi kilichopo katika kijiji cha Kamsisi Wilaya ya Mlele Mkoani Katavi, walikua wanaelekea nchini Afrika Kusini.

Mbinu hii mpya ya kutumia tanki la lori la mafuta na nyinginezo watakazobuni wahalifu wanaofanya biashara ya usafirisha wahamiaji haramu zinaonesha jinsi gani ugumu wa kupambana na tatizo hilo.

Chapisha Maoni

0 Maoni