WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya
Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kuboresha
huduma mbalimbali za kijamii nchini zikiwemo za afya, hivyo amewataka wananchi
waendelee kuipa ushirikiano.
Majaliwa ameyasema hayo jana, wakati akizungumza na wananchi
baada kuweka jiwe la msingi Hospitali ya Wilaya ya Newala akiwa katika ziara ya
kikazi mkoani Mtwara. Amesema kuwa Serikali imedhamiria kuendelea kuboresha
huduma za afya nchini.
Pia, Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Newala
asimamie ipasavyo upatikanaji wa dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya
kwa sababu Serikali inatoa fedha nyingi kwa ajili ya kugharamia huduma hiyo.
Waziri Mkuu amesema Serikali kila mwezi inapeleka fedha kwa
ajili ya ununuzi wa dawa hivyo hatarajii wananchi wanaokwenda kwenye vituo vya
kutolea huduma za afya wanakosa dawa. Amewasisitiza wapeleke dawa kulingana na
magonjwa yanayopatikana katika wilaya hiyo.
Awali, Mganga Mkuu wa Wilaya, Dk. Matiko George alisema
Serikali imetoa shilingi bilioni 2.85 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu
mbalimbali ikiwemo jengo la maabara, wagonjwa wa dharura, huduma ya mama na
mtoto, mionzi, utawala, wodi za wanawake, wanaume na watoto.
Alisema faida za mradi huo ni pamoja na punguzia gharama kwa
wananchi ambao walilazimika kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya katika
halmashauri za jirani za Newala Mji, Masasi na Hospitali ya Rufaa ya Ndanda.
“Hospitali hii itakuwa na uwezo wa kufanya huduma za upasuaji
kwa akina mama watakaokuwa wanapata changamoto ya kujifungua kwa njia ya
kawaida. Pia huduma za za afya za kinywa na macho nazo zitatolewa hospitalini
hapa,” alisema Dk. George.
Pia, Dk. George amemshukuru Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu
Hassan kwa kuendelea kuimarisha utoaji wa huduma za afya ikiwa ni pamoja na
kupeleka vifaa tiba vya kisasa katika hospitali za wilaya pamoja na vituo vya
afya jambo linalowaongezea ari ya kufanya kazi kwa bidii na kutoa huduma bora
kwa wananchi.
“Naipongeza Serikali kwa kuendelea kuboresha, kuimarisha na
kuongeza hali ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika hospitali na vituo
vya afya nchini. Vifaa tiba vilivyoko katika jengo la kutolea huduma za dharura
kwenye hospitali hii vinalingana na vile vinavyotumika katika hospitali ya
Taifa ya Rufaa ya Muhimbili,” alisema Dk. George.
CHANZO: Ofisi ya Waziri Mkuu
0 Maoni